Serikali
Kagera imeanza kuwapima watu wanaoingia kutoka nchi jirani kupitia mkoa
huu, ili kubaini kama wana maambukizi ya ugonjwa wa ebola.
Hatua hiyo inafuatia kutangzwa kwa mlipuko wa ugonjwa huo kaskazini magharibi mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Akizungumza
na waandishi wa habari katika Manispaa ya Bukoba jana, Kaimu Ofisa Afya
Mkoa wa Kagera, Geraz Ishengoma alisema kuwa kila mgeni anayeingia
nchini anapimwa na anayeonekana ana dalili zinazofanana na ugonjwa huo,
hupelekwa kupimwa zaidi.
Ni
mara ya pili katika mwaka mmoja kwa serikali kuchukua tahadhari dhidi
ya maambukizi ya ebola. Mei 29, mwaka jana Waziri wa Afya, Maendeleo ya
Jamii, Jinsi, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, alisema wageni kutoka nchi
hiyo wangesajiliwa na kufuatiliwa hadi wanakoishi ili kujiridhisha kama
hawana virusi vya ebola.
Kaimu
Ofisa Afya Mkoa wa Kagera, Ishengoma alisema jana: “Tumeweka kambi
katika maeneo ya mpakani hasa Mutukula, Murongo, Kabanga na Rusumo, (na)
kila mtu anayeingia anapimwa ikiwamo joto la mwili.
"Tunayekuwa na shaka naye, tunamtenga na kumchunguza zaidi.”
Alisema
kuwa kambi hizo za mpakani ziliwekwa baada ya serikali kutangaza kuwapo
kwa ugonjwa huo DRC Mei 8, mwaka huu, na kuwa hadi sasa hakuna mtu
yeyote aliyebainika kuwa na maambukizi ya virusi vya ugonjwa huo.
Alisema
virusi vya ugonjwa huo vinaambukizwa kwa kugusa damu au majimaji,
kugusa maiti ya mtu aliyekufa kwa ugonjwa huo na kugusa wanyama wenye
maambukizi, na kuwa dalili zake huanza kuonekana kuanzia siku mbili hadi
21 tangu mtu anapoambukizwa.
Ishengoma
alitaja dalili za ugonjwa huo kuwa ni homa kali, kulegea mwili, kichwa
kuuma kunakoambatana na kutapika na kutokwa na damu sehemu tofauti za
mwili, ikiwamo puani.
Kwa
upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Meja Jenerali mstaafu Salum Kijuu,
alisema serikali imechukua kila tahadhari ili kuhakikisha ugonjwa huo
hauingii nchini kupitia mkoa wa Kagera.
“Kumbukeni
Kagera ni mkoa ambao unapakana na nchi nyingi, zikiwamo za Rwanda,
Burundi na Uganda, lakini pia unapakana na mkoa wa Kigoma ambao watu
kutoka Congo hupitia katika mkoa huo na kuingia Kagera hasa kupitia eneo
la Murusagamba,” alisema.
Kijuu
aliwataka wananchi kutoa taarifa haraka endapo watabaini kuwapo kwa mtu
mwenye dalili kama za ebola katika maeneo yao, ili hatua za haraka
ziweze kuchukuliwa.
“Lakini
pia wananchi hawapaswi kugusana na mgonjwa mfano kugusa mate, majimaji
na damu, kuepuka kugusa maiti, kutochelewa kupata huduma na kuzingatia
usafi wa mwili,” alisema.
Alisema kuwa serikali inaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali, ili kuhakikisha ugonjwa huo hauingii nchini.