Mahakama ya Mji wa Kampala nchini Uganda, imempata na hatia mwanamke mmoja aliyejulikana kwa jina la Amina Mirembe (23) baada ya kukiri kosa la kujiteka makusudi kwa lengo la kupima upendo kwa mume wake.
Gazeti la Daily Monitor, limeripoti kuwa mwanamke huyo amehukumiwa leo Juni 5, 2018 kwa kutoa taarifa za uongo kwa Polisi kuhusu kutekwa kwake na Hakimu wa Mahakama hiyo Patrick Tulisana alimhukumu kwenda jela mwaka mmoja na kutoa kiasi cha shilingi za Uganda 300,000.
Mwendesha mashtaka wa serikali, Bi Lydia Batiibwe aliitaka Mahakama kutoa adhabu kali kwa mtuhumiwa Amina ili iwe fundisho kwa watu wanaotoa taarifa za uongo huku nchi hiyo ikikumbwa matukio mengi ya kujiteka makusudi
Mei 26, 2018 mshtakiwa aliandika maelezo ya uongo kwa Askari Polisi ASP Moses Acaye, katika eneo la Ntinda na kudai alikuwa ametekwa na watekaji hao walikuwa wakitaka shilingi za Uganda 500,000
Nchini Uganda kumekuwa na matukio ya watu kujiteka na kudai fedha kutoka kwa watu wa karibu, mathalani Juni 4, 2018 makahama eneo la Kayunga, ilimpata na hatia Bi Rebecca Birabwa (32) kwa makosa ya kujiteka na alihukumiwa kifungo cha miezi sita jela .