Mshambuliaji Lionel Messi ameanza vibaya Kombe la Dunia baada ya kukosa penalti huku Argentina ikilazimishwa sare 1-1 na Iceland katika mchezo wa kwanza wa Kundi D.
Messi alikosa penalti dakika 65, baada ya kipa wa Iceland, Halldorsson kuipangua.
Awali mshambuliaji Aguero aliangushwa na beki wa Iceland, Magnusson ndipo mwamuzi akatoa penalti hiyo.
Argentina ilianza mchezo huo kwa kasi na kufanikiwa kupata bao la kuongoza lililofungwa na Sergio Aguero kabla ya Iceland kusawazisha kupitia Alfreo Finnbogason.
Argentina ilitawala mchezo huo, lakini kikwazo kikubwa kwao alikuwa kipa Halldorsson aliyefanya kazi kubwa kuokoa hatari zote.
Iceland iliyocheza kwa nidhamu kubwa ya kujilinda muda wote mbinu yao ilifanikiwa na kuwafanya Argentina kushindwa kupata ushindi waliotegemea.