Pichani ni Marehemu Robert Muchangi baada ya kupigiliwa misumari kichwani.
Mwanaume aliyefahamika kama Robert Muchangi aliyepigiliwa misumari miwili na bosi wake kichwani nchini Kenya amefariki jana Juni 22 katika hospitali ya taifa ya Kenyatta.
Muchangi alifariki katika hospitali ya taifa ya Kenyatta alipokuwa amelazwa katika chumba cha wagonjwa mahututi baada ya kukumbwa na kisanga hicho mjini Meru, ambapo alitendewa unyama huo baada ya kwenda kumdai fedha walizokubaliana baada ya kumjengea nyumba Bosi wake huyo.
Familia ya Muchangi imesikitishwa na tukio hilo kwa kile walichodai kuwa Polisi wamekaa kimya, Dada wa marehemu anayejulikana kama Regina Murugi amesema kuwa tukio hilo limeleta pigo kwenye familia.
“Kaka yangu amefanyiwa unyama huu lakini kwasababu ya hali yetu duni askari hawana msaada wowote kwetu, kaka alikuwa ndio kila kitu kwakweli ametuachia mzigo mkubwa sana”, amesema Regina.
Muchangi ameacha bili ya zaidi ya Shilingi Milioni 6 za Kitanzania katika hospitali hiyo ambazo ndugu zake wanatakiwa wazilipe, ndugu zake Muchangi wamelilalamikia jeshi la Polisi nchini humo kwa kukaa kimya juu ya tukio hilo.
Muchangi ametendewa tukio hilo mnamo Juni 13, 2018 kwenye kichwa chake katika eneo la Igembe Nchini Kenya, ambapo misumari hiyo ilitoboa fuvu la kichwa chake.
Chanzo: Standard Digital