Mbunge wa Manispaa ya Arua nchini Uganda (MP), Ibrahim Abiriga ameuawa kwa kupigwa risasi karibu na nyumba yake huko Mattuga Wilaya ya Wakiso.
Alidaiwa kupigwa risasi na watu wawili waliokuwa wakiendesha boda boda mwendo wa saa kumi na mbili na nusu siku ya Ijumaa Juni 8,2018.
Mlinzi wake aliyekuwa akindamana naye pia alipigwa risasi katika gari lake.
Alikuwa mmoja wa viongozi walioshinikiza kubadilishwa kwa katiba kuondoa kifungu cha 102b ili kuweza kuondoa kikomo cha umri wa rais cha miaka 75 kuondolewa.
Hatahivyo hatua yake ya kutaka kikomo hicho kuondolewa ilisitishwa na kesi mahakamani baada ya kutuhumiwa kukojoa katika eneo la umma karibu na makao makuu ya wizara ya fedha mjini kampala.
Abiriga baadaye alipigwa faini ya shilingi 40,000 za Uganda na mahakama ya barabarani ya Buganda kwa kuwa msumbufu wa umma.
Katika eneo la Matugga, maafisa wa polisi na maafisa wengine wa usalama wamelizunguka eneo la kisa hicho ili kuhakikisha kwamba halivurugwi.
Abiriga ambaye masomo yake yametiliwa shaka na wapinzani wake wa kisiasa hivi majuzi alipokea cheti cha Diploma kutoka kwa Taasisi ya Nile mjini Arua.
Tayari rais wa taifa hilo Yoweri Museveni ameagiza vitengo vya usalama kuwatafuta wauaji wa kiongozi huyo .
Katika mtandao wake wa Twitter Museveni alimuomboleza mbunge huyo akisema kuwa waliotekeleza kitendo hicho wana roho ngumu.
''Nimepokea habari kuhusu mauaji ya kinyama ya mbunge wa Manispaa ya Arua , mheshimiwa Ibrahim Abiriga na mlinzi wake nje ya mji wa Kampala.
Nimeviagiza vitengo vya usalama kuwasaka waliotekeleza kitendo hicho na taifa litajuzwa hivi karibuni'', aliandika Museveni.
Chanzo- BBC