Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchikavu na Majini (Sumatra) imepanga kuondoa daladala zote zinazosafirisha abiria katika 'ruti' zote za Jiji la Mwanza, mwakani.
Akizungumza jijini hapa, Mkurugenzi Mkuu wa Sumatra, Gilliard Ngewe, alisema mamlaka hiyo imeanzisha mfumo mpya wa usafiri ambapo wamiliki wa daladala zitoazo huduma sasa jijini hapa wanatakiwa kuungana ili kutoa huduma hiyo kwa kutumia mabasi makubwa ya usafirishaji kupitia ama kampuni au ushirika.
Ngewe alikuwa akizungumza wakati wa mafunzo ya siku moja ya elimu juu ya utoaji wa huduma ya usafirishaji mijini, kwa kuziondoa daladala na kutumia usafiri wa mabasi makubwa.
"Serikali imechukua hatua madhubuti ya kusimamia wamiliki wa daladala kuhakikisha wanaunganisha mitaji yao na kununua mabasi makubwa ya kutoa huduma katika jiji hili la Mwanza kupitia makampuni (kampuni) au ushirika," alisema Ngewe.
"Tunatarajia kufikia mwakani 2019 (mwakani) daladala zote ziwe zimeondolewa katika jiji hili na kuanza kutumia mabasi makubwa yenye kubeba abiria wengi kwa mara moja."
Ngewe alisema kuanzishwa kwa mfumo huo mpya jijini Mwanza kutaondoa changamoto ya msongamano wa magari unaosababishwa kwa kiasi kikubwa na daladala.
Alisema jiji hili lina wamiliki wa daladala zaidi ya 2,000 na idadi ya magari 3,400 yanayotoa huduma hiyo.
Kama mpango huo utatekelezeka, ndani ya miezi sita ijayo Mwanza litakuwa jiji la pili nchini kuondoa huduma ya usafiri wa daladala baada ya Dar es Salaam iliyozipunguza kwa kiasi kikubwa katika Barabara za Morogoro na Kawawa mwaka 2016.
Katika njia hiyo, jiji hilo limeweka mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART).
Ngewe alisema mfumo mpya huo kwa Mwanza utasaidia pia madereva na makondakta wa daladala za sasa kupata mikataba ya kisheria ya ajira zao na kulipwa mishahara na mafao ya uzeeni pindi wanapostaafu kazi.
Ngewe alisema mabasi makubwa yatakayokuwa yakitoa huduma hizo yatatumia mfumo wa kielektroniki katika utoaji wa tiketi kwa abiria.
Aidha, mfumo wa kielektroniki utaondoa wizi wa fedha za makusanyo ya nauli za wenye magari unaofanywa na madereva na makondakta wasio waaminifu, alisema.
Ngewe alisema mfumo wa kuungana mitaji kwa wamiliki kupitia kampuni au ushirika ili kuendesha biashara ni mzuri kwani utawasaidia kupata mikopo ya kifedha kwa urahisi, kukuza mitaji na uchumi kuliko umiliki wa mtu mmoja mmoja.
Mafunzo hayo yalihusisha viongozi wa usalama barabarani, wamiliki wa daladala za abiria mijini, viongozi wa Chama cha Kutetea Abiria (Chakua) na wadau mbalimbali wa usafirishaji kutoka mikoa ya Kanda ya Ziwa.
Credit: Nipashe
Social Plugin