Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

DC NDAGALA AWAKALIA KOONI WAKANDARASI WAZEMBE KAKONKO


Kutokana na kusuasua na kutokamilika kwa wakati katika miradi ya maji wilayani Kakonko mkoani Kigoma mkuu wa wilaya ya Kakonko Kanali Hosea Ndagala ameanza kuwachukulia hatua wakandarasi wote ambao mpaka sasa wameshindwa kufikia asilimia 25% ya miradi hiyo.

Mkuu huyo wa wilaya ameagiza mkandarasi huyo akamatwe kutokana na udanganyifu alioufanya na kuwaagiza wakandarasi wa miradi mitatu katika vijiji vya Gwanumpu, Kakonko na Nyabibuye iliyotengewa kiasi cha shilingi bilioni 1.2 kwa ajili ya kuondoa kero ya maji katika vijiji hivyo kukamilisha asilimia 25 % ya miradi hiyo ndani ya wiki mbili na wasipofanya hivyo watachukuliwa hatua ikiwa ni pamoja na kunyang'anywa miradi hiyo.

Kanali Ndagala amefikia hatua hiyo jana baada ya kutembelea miradi hiyo na kubaini kuwepo kwa udanganyifu mkubwa kwa baadhi ya wakandarasi akiwemo Malack Kishulugwa mkandarasi wa maji anayetekeleza mradi katika kijiji cha Nyabibuye ambaye mara baada ya kusaini mkataba alitoweka katika eneo la kazi na kurejea jana baada ya kupata taarifa mkuu wa wilaya kutembelea mradi huo.

Mradi huo uliosainiwa mnamo 27 Machi,2018 na kutakiwa kukamilika Septemba 6,2018 ukiwa na thamani ya shilingi milioni 650 unatarajiwa kuwahudumia zaidi ya wakazi 4713 wa vitongoji saba vya kijiji cha Nyabibuye ambao sasa wanafuata maji umbali wa kilomita 7 baada ya mradi uliokuwepo kuacha kutoa maji kutokana na miundombinu kuharibika.

"Wakandarasi hawa wamepewa kazi hii tangu mwezi Machi na mwezi Septemba wananchi wanatakiwa kuanza kupata maji katika miradi hii lakini baadhi yao hwajaanza hata kujenga eneo la kuhifadhia vifaa kutokana na waliposaini mikataba yao waliondoka, sasa nimegundua miradi ya Kakonko inashindwa kukamilika kwa kuwa wakandarasi wengi sio waaminifu sasa nitoe wito kwa wote wanaoomba kufanya kazi Kakonko wawe makini wananchi wanahitaji maji na wao wanatakiwa wafanye kazi hatutawavumilia wanaokwamisha maendeleo yetu", alisema Ndagala.

Akijitetea mbele ya mkuu wa wilaya, mkandarasi huyo Malack Kishulugwa alisema changamoto zilizomfanya ashindwe kufanya kazi hiyo ni mvua zilizokuwa zikinyesha na kuahidi kukamilisha ujenzi wa matenki, uchimbaji wa mitaro na ufyatuaji wa matofali ndani ya wiki mbili. 

Diwani wa kata ya Nyamibuye Steven Mnigakikwa alisema kwa sasa wananchi wanapata adha kubwa ya upatikanaji wa huduma ya maji kijijini hapo ambapo awali mradi uliokuwepo miundo mbinu yake imechakaa na hivyo halmashauri kuamua kuanzisha mradi wa ujenzi wa matanki na kupata chanzo kipya cha maji lengo likiwa ni kupunguza adha kwa wananchi ndani ya kaya ya Nyamibuye yenye vitongoji kumi na mbili.

Alisema mkandarasi anayetekeleza mradi katika kijiji hicho alitoweka eneo lake la kazi kwa muda wa takribani siku 42 jambo lililowakatisha tamaa wananchi ya kupata maji lakini pia mkandarasi huyo amekuwa akiendelea kutoa kauli za uongo mbele ya mkuu wa wilaya kwa madai ya kunyesha kwa mvua na imekuwa chanzo cha yeye kushindwa kufanya shughuli zake jambo ambalo si sahihi mvua ilikata muda mrefu tangu mwezi Mei mwishoni.

"Katoa ahadi ya kuanza kutekeleza mradi haraka iwezekanavyo na ndani ya wiki mbili atakuwa amekamilisha sehemu ya mradi, hivyo tunasubiri kuona na endapo hata tekeleza basi kama halmashauri tutachukua hatua ikiwemo ya kuvunja mkataba", alisema Mnigakinko.

Kaimu mwenyekiti wa kijiji cha Nyamibuye John Nyabumbwe alisema tatizo la maji kijijini hapo ni kubwa ambapo wananchi wanalazimika kutembea umbali wa kilomita saba kufuata huduma ya maji na kusababisha baadhi ya kazi zao walizoziacha nyumbani kukwama kutokana na foleni kubwa iliyopo katika eneo wanalochotea maji.

Alisema wananchi walitarajia kukamilika kwa mradi wa maji itakuwa chachu ya kuwapunguzia adha ya kutafuta maji lakini hadi sasa wananchi wamekata tamaa kutokana na mkandarasi kushindwa kufika eneo lake la kazi na kufanya shughuli zake na hakuna uhakika kama mwaka huu wananchi watapata huduma ya maji kitokana na kusuasua kwa mradi.

Mmoja wa wananchi Liberata Jacksoni alisema adha ya maji inaathiri shughuli zao za nyumbani na kuhatarisha ndoa zao kutokana na kukaa muda mrefu kisimani kusubiri maji na hivyo kuiomba serikali kuwapatia msaada wa maji katika maeneo yao.

Na Rhoda Ezekiel - Malunde1 blog 

Mkuu wa wilaya ya Kakonko Kanali Hosea Ndagala akikagua miradi ya maendeleo








Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com