Wananchi wa vijiji vya Kinyinya na Nyagwijima kata ya Mgunzu wilayani Kakonko Mkoani Kigoma wametakiwa kushirikiana na viongozi wa kata na vijiji kujenga nyumba za askari polisi ili kupunguza vitendo vya utekaji katika eneo la Kosovo wilayani humo.
Akizungumza katika mkutano wa kusikiliza kero za wananchi na kuhamasisha maendeleo kwa wananchi wa kata hiyo jana, Mkuu wa Wilaya ya Kakonko Kanali Hosea Ndagala alisema katika wilaya ya Kakonko masuala ya utekaji yamepungua lakini yamebaki katika maeneo machache ambayo hayafikiki kiurahisi na kuwahimiza wananchi kutoa ushirikiano kujenga nyumba za askari waweze kukaa katika eneo hilo na kukomesha vitendo hivyo.
Alisema wananchi wanatakiwa kujitoa kwa michango pamoja na kujitoa wenyewe kujenga, kwa kuwa wanaotekwa na kuporwa mali zao ni wananchi wenyewe na kwa vile serikali inatoa msaada mkubwa wa kuleta maendeleo kwa wananchi na wananchi wanatakiwa kujitoa katika vijiji vyao kutokomeza vitendo hivyo.
"Mimi niwaombe viongozi wa vijiji muendelee kuhimiza suala hili la kujenga nyumba za askari katika eneo la Kosovo... eneo hili ni eneo ambalo watu wanatekwa muda wa saa kumi na mbili jioni ambapo kuna uwezekano wa kuzuia hili....
Kwa wilaya ya Kakonko na mkoa kwa ujumla tumejitahidi kukomesha vitendo vya utekaji na jeshi la polisi linafanya kazi kubwa sana na juhudi zinaonekana wananchi na viongozi msitukwamishe kwa hili", alisema mkuu huyo.
Hata hivyo Mkuu huyo wa wilaya aliwataka wananchi kuwapuuza wale wote wanaowadanganya na kuwashawishi wasijitolee kuleta maendeleo na kujitoa katika kujenga miradi ya maendeleo katika vijiji vyao kwa kuwa maendeleo ya wananchi yanaletwa na wananchi wenyewe.
Nae Diwani wa kata ya Mgunzu Andrea Mashama alisema mpaka sasa wanaendelea kuhimiza wananchi kujitolea na tayari wameitisha mkutano wa wananchi na wenyeviti wa vijiji nawamefikia muafaka wa kila mwananchi kuchangia shilingi elfu moja.
Alisema kwa sasa wananchi wanaendelea kuchangia na kujenga nyumba ya mganga na kituo cha afya na kufanya shughuli zingine za maendeleo kwa wananchi wote wa vijiji vya Kinyinya na Nyagwijima.
Kwa upande wao baadhi ya wananchi akiwemo Joachim Joram walisema wao kama wananchi wanaumia sana wanapotoka mashambani na kuibiwa mazao pamoja na fedha zao hali ambayo inawarudisha sana nyuma kimaendeleoo na kumuahidi mkuu huyo kuwa watafanikisha suala hilo na kukomeshwa kwa suala hilo.
Mkuu wa Wilaya ya Kakonko Kanali Hosea Ndagala akizungumza na wananchi - Picha na Rhoda Ezekiel - Malunde1 blog Kigoma
Social Plugin