Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro amewataka wakulima wa zao la pamba kufuata masharti ya kilimo cha zao hilo kutoka kwa watalaamu kuanzia maandalizi hadi kwenye upuliziaji wa dawa ya kuua wadudu jambo ambalo litawafanya kupata mavuno mengi na kuinuka kiuchumi.
Matiro alibainisha hayo juzi Juni 23,2018 alipofanya ziara ya ukaguzi wa uuzwaji wa zao la pamba katika kijiji cha Sayu kata ya Pandagichiza Shinyanga vijijini na kupokea malalamiko kutoka kwa wakulima wa zao hilo kuwa dawa ambazo wameuziwa na serikali zile mpya Dudu ba na Dudu o ni feki haziui wadudu na hatimaye kuwa tia hasara kwa kupata mavuno kidogo.
Matiro alisema ili mkulima ainuke kichumi kupitia zao hilo la pamba ni lazima afuate masharti ya kilimo hicho kutoka kwa watalaamu kwa kulima kisasa pamoja na kuzingatia kupulizia kwa ufasaha wa dawa za kuua wadudu hao na siyo kwenda kinyume chake.
“Nawataka wakulima wa zao la pamba mfuate masharti ya kilimo hiki kutoka kwa wataalamu wetu ndipo mtapata faida zaidi kwa kupata mavuno mengi na kuinuka kiuchumi, achaneni na kilimo cha kizamani ambacho hakina tija”,alisema Matiro.
“Suala hili la madai kuwa dawa hizi mpya ni feki serikali imelichukua na itakwenda kulifanyia kazi, ikiwa lengo ni kutaka kurudisha heshima ya zao la pamba pamoja na kumuinua mkulima kiuchumi,”aliongeza.
Nao wakulima wa zao hilo la Pamba katika kijiji hicho walisema asilimia kubwa ya wakulima walifuata masharti ya kilimo hicho isipokuwa tatizo lililo waangusha ni dawa kutokuwa na nguvu ya kuua wadudu na hivyo kuwatia hasara.
Mmoja wa wakulima hao Felician Shija alisema katika mavuno ya pamba hekali kumi wameambulia kuvuna kilo 300 pekee, ambapo matarajio yalikuwa ni kuvuna kilo 2,000 hadi 3,000 na hivyo kuiomba serikali iwarudishie dawa za zamani ambazo zilikuwa zikiua wadudu vizuri kuliko hizo mpya.
Naye Andrew Maganga alisema baada ya kuona dawa hizo haziui wadudu akaamua kuelekeza nguvu kwenye shamba lake moja lenye hekali tatu na nusu na kwenda kinyume na maagizo ya watalamu ya upuliziaji wa dawa hizo na kuamua kuzidisha vipimo pamoja na kuingia shambani mara kwa mara hali ambayo imemsaidia kupata mavuno mazuri kiasi.
Kwa upande Ofisa kilimo wa halmashauri ya wilaya ya Shinyanga vijijini Edward Maduhu alisema wadudu hao walishindwa kufa kutokana na mabadiliko ya tabia nchi, ambapo mvua zilikithiri kunyesha kwa wingi na mkulima anapo pulizia dawa hizo hukosa nguvu huku akibainisha kuwa baadhi yao pia hukosea masharti ya upulizaji dawa.
TAZAMA MATUKIO KATIKA PICHA HAPA CHINI
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro akiwa kwenye Shamba la Pamba la Mkulima Andrew Maganga katika kijiji hicho cha Sayu na kuwataka wakulima wengine waige mfano wake wa kuwa mbunifu kukabiliana na wadudu waharibifu wa zao la pamba na hatimaye kupata mavuno mengi.Picha zote na Marco Maduhu - Shinyanga
Mkuu wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro akiendelea na ukaguzi wa zao la pamba shambani.
Mkulima wa zao la Pamba Andrew Maganga akielezea namna alivyoamua kuwa mbunifu kwa kukabiliana na wadudu, ambapo aliamua kwenye kinyume na wataalamu kwa kuzidisha vipimo vya dawa na kuingia shambani mara kwa mara kupulizia dawa ya kuua wadudu na hatimaye kupata mavuno mazuri ya zao hilo.
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro akiwasisitiza wakulima wa zao hilo la pamba kujitahidi kuzingatia kufuata masharti ya kilimo cha zao hilo la pamba kutoka kwa wataalamu ili wapate mavuno mengi na kuinuka kiuchumi.
Kushoto ni Ofisa Kilimo wa kata ya Pandagichiza Heda Kalume akimwelezea mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro, namna msimu wa ununuzi wa zao la pamba unavyokwenda kuwa una hali nzuri na hakuna changamoto yoyote.
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro akisikiliza kero za wakulima wa zao la pamba katika kijiji cha Sayu kuwa tatizo ambalo limekuwa changamoto kwao ni dawa za kuulia wadudu ambazo hazina nguvu na hivyo kuwapatia hasara ya kupata mavuno kidogo tofauti na matarajio.
Wakulima wa zao la Pamba wakiwa kwenye kituo cha kuuzia pamba kwenye Kijiji cha Sayu ambapo tela hilo wamedai limebeba kilo 300 kutoka kwenye Shamba la hekali 10, ambapo zao hilo lisingeshambuliwa na wadudu wangeweza kupata kilo 2,000 hadi 3,000 na hivyo kuiomba serikali iwarudishie dawa za zamani.
Ofisa Kilimo wa Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga Vijijini Edward Maduhu akieleza kuwa wadudu hao walishindwa kufa kutokana na mabadiliko ya tabia nchi, ambapo mvua zilikithiri kunyesha kwa wingi na hivyo mkulima akipulizia dawa hukosa nguvu na wadudu kushindwa kufa, huku baadhi ya wakulima wakishindwa kufuata masharti ya kupulizia dawa.
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro akijibu kero za wakulima wa zao hilo la pamba, na kuwa hakikishia kuwa Serikali imelichukua suala hilo la dawa na kwenda kulifanyia kazi, lengo likiwa na kurudisha heshima ya zao la pamba na kumuinua kiuchumi mkulima.
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro akiwa katika ziara ya ukaguzi wa uuzwaji wa zao la pamba katika kijjiji cha Sayu kupitia vyama vya Ushirika, na ukaguzi wa mashamba ya zao hilo.
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro akiwa kwenye shamba la pamba akiongea na wakulima wa zao hilo namna ya kufuata masharti yake, na kuwainua kiuchumi.
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro akiwa na Diwani wa kata ya Solwa Awadhi Abood alipofanya ziara pia kwenye Zahanati ya Solwa.
Mganga wa Zahanati ya Solwa akielezea ujenzi wa Wodi namna ulivyofikia.
Katibu tawala wa wilaya ya Shinyanga Boniphace Chambi akiangalia ujenzi wa Wodi katika zahanati ya Solwa Shinyanga vijijini.
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro akipongeza wanaume wa Kata hiyo ya Solwa kwenda na wake zao kwenye Zahanati hiyo kupewa ushauri Nasaha namna ya kumhudumia mtoto tangu akiwa tumboni.
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro akiendelea na pongezi kwa wanaume kwenda na wake zao katika zahanati ya Solwa kupatiwa ushauri Nasaha na kutoa wito kwa wanaume wengine kuiga mfano huo.
Pongezi zikiendelea.
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro akizungumza na wananchi wa Kata ya Solwa waliofika kupewa ushauri kwenye zahanati hiyo na kuwataka wazingatie ushauri huo ambao utawasaidia kujifungua watoto wenye afya njema.
Picha zote na Marco Maduhu - Shinyanga
Social Plugin