Mwenyekiti wa Kamati Maalum ya Bunge iliyochunguza masuala ya Gesi Asilia, Dunstan Kitandula akitoa taarifa ya kamati hiyo iliyoundwa na Spika wa Bunge, Job Ndugai kabla ya kumkabidhi katika Viwanja vya Bunge, jijini Dodoma leo. Spika aliunda kamati hiyo ili kumshauri kuhusu masuala hayo. Picha na Edwin Mjwahuzi
****
Mwenyekiti wa Kamati Maalum ya Bunge ya Gesi Asilia, Dunstan Kitandula amesema wamebaini madudu yanayoisababisha Serikali hasara ya Sh291bilioni sawa na bajeti ya wizara nne, akiwemo mfanyakazi mmoja wa kampuni ya Payeti anayelipwa mshahara wa Sh96 milioni kwa mwezi.
Hayo yamebainishwa na kamati hiyo iliyochunguza uvuvi wa bahari kuu na gesi asilia iliyoundwa na Spika Job Ndugai ambayo leo Jumamosi Juni 2, 2018 imewasilisha taarifa yake ya uchunguzi kwa kiongozi huyo wa Bunge mjini Dodoma.
Akizungumza wakati wa makabidhiano ya taarifa za kamati hiyo, Kitandula amesema walibaini kuwepo kwa baadhi ya wafanyakazi kutoka nje ya nchi wanaolipwa mishahara mikubwa kwenye kampuni hizo ikilinganishwa na Watanzania.
Amesema kuwepo kwa baadhi ya masharti kwenye mikataba ya gesi asilia yasiyo na tija yoyote kwa Taifa na badala yake yanalisababisha hasara.
Ameeleza kuwa dosari walizobaini kwenye mikataba hiyo zinaisababishia Serikali hasara ya zaidi ya Sh291 bilioni sawa na bajeti ya wizara nne.
Amebainisha kuwa ripoti hiyo amesema baadhi ya wafanyakazi wageni kwenye kampuni zinazofanya kazi hiyo wanalipwa mishahara mikubwa ikilinganishwa na wale wa ndani.
Ametaja baadhi ya masharti kikwazo kuwa ni tozo na ada mbalimbali, vifungu vinavyolazimisha akaunti za kampuni hizo kufunguliwa nje ya nchi na utaratibu wa kutatuliwa migogoro nje ya nchi na sharti.
Chanzo- Mwananchi