ZAIDI ya makachero 20 wa Jeshi la Polisi waliovalia kiraia, wamefika katika Shule ya Msingi St. Florence Academy, kuchunguza sakata la mwalimu anayetuhumiwa kudhalilisha wanafunzi wa kike kwa kuwapapasa sehemu zao za siri.
Makachero hao walifanya mahojiano na uongozi wa shule, walimu, wanafunzi na wafanyakazi wa shule hiyo, juu ya tuhuma hizo zinazomkabili mwalimu anayejulikana kwa jina la Ayoub Mlubu, anayedaiwa kuwafanyia vitendo hivyo wanafunzi wanne wa darasa la saba.
MTANZANIA ikiwa shuleni hapo asubuhi jana, ilishuhudia kundi la kwanza la makachero wakiwa shuleni hapo, wengine wakimhoji Mkuu wa shule hiyo, Mwalimu Wilson Mwabuka.
Wakati mahojiano hayo yakiendelea, makachero wengine walionekana wakirandaranda kwenye maeneo ya shule hiyo.
Ilipofika saa 7:56 mchana, Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Salum Hapi, alifika na kwenda moja kwa moja kwenye ofisi ya mkuu wa shule ambayo ndani ilikuwa haina mtu.
Alipoona hivyo, akaamua kwenda kwenye ofisi nyingine za walimu ili aweze kuzungumza nao, lakini baadhi yao walipomuona, walimkimbia na kuingia ndani ya madarasa na kufunga milango.
Alipoendelea kuwafuata walimu hao, waliendelea kukimbia na kufunga milango kila walipokuwa wanaingia madarasani.
Hali hiyo ilimfanya Hapi kuzunguka kwenye majengo mbalimbali ya shule hiyo kutafuta viongozi, na baadaye alionana na mwalimu Mwabuka ambaye alikuwa kwenye moja ya madarasa.
Mwalimu huyo alimchukua na kumpeleka ofisini kwake na baada ya dakika chache, walitoka na kuelekea ofisi ya mkurugenzi.
PATRICIA KIMELEMETA NA TUNU NASSOR – Dar es Salaam
CHANZO-MTANZANIA