Mbunge wa Mbeya Mjini (Chadema), Joseph Mbilinyi maarufu kama Sugu amesema wakati wowote kuanzia sasa anatarajia kuachia wimbo wake mpya alioupa jina la 219, ambayo ni namba yake aliyopewa wakati akitumikia kifungo cha miezi mitano katika Gereza Kuu la Ruanda, Mbeya.
Sugu ambaye ni msanii wa Hiphop anaachia wimbo huo ikiwa zimepita siku 25 tangu alipotoka gerezani kwa msamaha wa Rais John Magufuli, Mei 10, 2018.
Akizungumza na MCL Digital leo Jumapili Juni 3, 2018, Sugu amesema maandalizi yote yamekamilika, “maandalizi na kila kitu kipo poa na soon (muda si mrefu) nitautoa wimbo wangu nilioupa jina la 219.”
“Nimeimba mimi mwenyewe wimbo na nimezungumzia hali ya nchi, experience (uzoefu) yangu niliyoipata gerezani na mambo mengine, ni ngoma nzuri kabisa.”
Alipoulizwa sababu za wimbo huo kuupa jina la namba yake ya mfungwa amesema, “kwa kuwa hii ni namba inajulikana nchi nzima na kwa kuwa wanaitambua, tunawapelekea wimbo kupitia hii namba.”
Sugu amesema alipokaa gerezani amejifunza mambo mengi na kupitia majukwaa yake mawili ya siasa na muziki, atayatumia kufikisha ujumbe kwa wananchi.
“Namshukuru Mungu mimi nina majukwaa mawili, nikiona katika siasa kazi natumia jukwaa la muziki kufikisha ujumbe. Kwa hiyo wakibana katika siasa napiga muziki,” amesema.
Na Ibrahim Yamola, Mwananchi
Social Plugin