Mchezaji wa zamani Misri na mtangazaji wa Michezo amepoteza maisha baada ya kuugua ugonjwa wa moyo kwenye mchezo wa Saudi Arabia na Misri katika michuano ya kombe la Dunia inayoendelea nchini Urusi.
Abdel Rahim Mohamed ambaye aliwahi kuifundisha klabu ya Zamalek aliugua ugonjwa huo usiku wa Jumatatu baada ya timu yake ya taifa ya Misri kupoteza 2-1 katika mchezo wa mzunguko wa tatu hatua ya makundi ya kombe la Dunia ilipocheza na Saudi Arabia ambapo goli hilo la pili la Saudi Arabia lilifungwa katika dakika ya 90+5.
Inadaiwa Abdel Rahim alianza kuugua ugonjwa wa moyo kabla ya kuanza kwa michuano hiyo ambapo yeye alikabidhiwa kutangaza mechi za kundi A katika chaneli moja nchini humo ambalo timu ya Taifa ya Misri ilikuwemo.
Katika jitihada za kuokoa maisha yake, alikimbizwa katika Hospitali ya Qasr Al-Aini ambako alipewa matibabu kwa muda wa nusu saa kabla ya kupoteza maisha.
Ahmed Fawzi ambaye ni Mlinda Mlango wa zamani aliyekuwepo pamoja naye studio wakati wa tukio hilo alieleza kuwa Abdel Rahim alionekana kuathiriwa kwa kiasi kikubwa na matokeo hayo ya kipigo cha tatu cha Misri katika michuano hiyo ambayo imeshiriki kwa mara ya kwanza tangu 1990 .
Katika kundi A, Misri na Saudi Arabia zimeondolewa katika michuano hiyo huku wenyeji Uruguay na Urusi zikisonga mbele katika hatua ya 16 bora ambapo Uruguay itavaana na Ureno na Urusi itakutana na Hispania.