Mkuu wa Mkoa Mwanza Mhe.John Mongella akizungumza kwenye kikao kazi na viongozi mbalimbali wa elimu mkoani Mwanza kilichofanyika jana Mei 31, 2018 katika chuo cha ualimu Butimba.
Na George Binagi-GB Pazzo, BMG
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza John Mongella ametoa zawadi ya shilingi milioni moja kwa mkuu wa shule ya msingi Kazunzu iliyopo halmashauri ya Buchosa wilayani Sengerema Mwl.Augustine Masesa baada ya shule yake kufanya vizuri kwenye matokeo ya darasa la saba kwa miaka miwili mfululizo kuanzia 2016.
RC Mongella alitoa zawadi hiyo jana wakati akizungumza kwenye kikao kazi kilichowajumuisha maafisa elimu taaluma ngazi ya mkoa, maafisa elimu msingi na sekondari ngazi ya wilaya, wadhibiti ubora ngazi ya wilaya, waalimu wakuu wa serikali na binafsi pamoja na makatibu wa TSC ngazi ya wilaya.
Aidha RC Mongella alitoa ahadi ya shilingi milioni tano baada ya mwalimu huyo kuahidi shule yake kuwa ya kwanza kiwilaya, kimkoa na tano bora kitaifa kwenye matokeo ya darasa la saba mwaka huu huku akimwagiza Afisa Elimu mkoani Mwanza kumpandisha cheo mwalimu huyo kuwa Afisa Elimu Kata.
Pia Afisa Elimu mkoani Mwanza Mwl.Michael Ligola alitoa motisha ya shilingi laki mbili kwa mwalimu huyo na kubainisha kwamba kikao kazi hicho kililenga kuimarisha hali ya ubora wa elimu ikiwemo ufaulu.
Katika matokeo ya darasa la saba mwaka 2016 shule ya msingi Kazunzu ilishika nafasi ya kwanza kiwilaya, ya tatu kimkoa na ya 28 kitaifa hii ikiwa ni kwa shule zote za serikali na binafsi na kwa shule za serikali ikishika nafasi ya kwanza kitaifa.
Mwaka 2017 ilishika nafasi ya kwanza kiwilaya, ya tatu kimkoa na ya 25 kitaifa kwa matokeo ya shule zote za serikali na binafsi na ya kwanza kitaifa kwa shule za serikali ambapo jana alipata fursa ya kuelezea siri ya mafanikio hayo.
Afisa Elimu mkoani Mwanza, Mwl.Michael Ligola akizungumza kwenye kikao hicho.
Mkuu wa shule ya msingi Kazunzu, Mwl.Augustine Masesa akiwa kwenye kikao hicho.
Viongozi mbalimbali wa elimu mkoani Mwanza.