Naibu Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson amewataka wabunge kuacha visingizio kuwa mashine za kupimia virusi vya Ukimwi (VVU) ni vibovu na badala yake wajitokeze kwa wingi kupima afya zao.
Kauli hiyo imetolewa leo Juni 21, 2018 baada ya Spika wa Bunge, Job Ndugai kuzindua kampeni ya kupima VVU kwa wabunge na watumishi wa muhimili huo katika viwanja vya Bunge mjini hapa.
“Nimepata kikaratasi hapa kutoka kwa mmoja wa wabunge kuwa mashine ya kupima (VVU) ni mbovu, mashine ni nzima nendeni mkapime. Mimi tayari nimeshapima,”amesema Dk Tulia.
Awali akiwahamasisha wabunge waende kupima VVU, Dk Tulia amesema Mbunge wa Nkasi Kaskazini (CCM), Ally Keissy alikuwa wa kwanza kwenda kupima VVU na tayari amepokea majibu yake.
Mara baada ya kupima VVU, Spika Ndugai amewataka watu kuacha kuogopa kwenda kupima kwa sababu watafanya hivyo kwa faragha na wataweza kuishi maisha yenye furaha.
Mwenyekiti wa Baraza la Watu Wanaoishi na Virusi vya Ukimwi (Nacopha), Justine Mwinuka amesema kupima afya kwa wabunge na viongozi wengine katika jamii kutasaidia kuondoa woga unaotokana na hofu ya kunyanyapaliwa.
Na Sharon Sauwa, Mwananchi
Social Plugin