Vijana wanaohitimu mafunzo ya awali ya kujitolea ya oparesheni Mererani ya Jeshi la Kujenga Taifa JKT katika kambi ya Bulombola 821KJ wametakiwa kuwa mfano wa kuigwa na jamii wanayoenda kuishi nayo pamoja na kujikita katika shughuli za uzalishaji mali ili kufikia adhma ya Rais wa serikali ya awamu ya tano Dr John Pombe Magufuli kuifikisha Tanzania katika uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025 na kuwa Tanzania ya viwanda.
Wito huo ulitolewa jana na Mkuu wa wilaya ya Buhigwe Brigedia Jenerali Marko Gaguti katika sherehe za kuhitimu mafunzo ya awali ya Kijeshi katika kambi hiyo wilayani Kigoma mkoani Kigoma na kuwataka vijana hao kutumia stadi za kazi wanazofundishwa na kuwa mfano kwa vijana wengine na kusaidia serikali kufikia uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.
Brigedia Jenerali Gaguti alisema mafunzo waliyoyapata vijana hao yanawafanya kuwa wazalendo na vijana wanaojishughulisha na shughuli mbalimbali za maendeleo na kutoa wito kuwa mafunzo hayo waliyoyapata wayatumie kujijenga kiuchumi na kujiajiri wenyewe ili kuweza kuanzisha viwanda na kuwa na uchumi wa kati.
“Nitoe rai vijana mlio hitimu mafunzio haya muwe vijana mnaowaza mtaifanyia nini Tanzania na sio Tanzania iwafanyie nini, na vijana wenye uthubutu mtakaosaidia kutoa suluhu kwa changamoto ya vijana nchini na sio kuwa sehemu ya matatizo ya vurugu na mtoe darasa kwa vijana wengine kufanya matendo mema,’’alisema Jenerali Gaguti.
Kwa upande wake Kamanda wa kikosi cha 821KJ kambi ya Bulombola Luteni Kanali Rashidi Kanole alisema vijana waliohitimu mafunzo hayo ya oparesheni Mererani ni vijana 839 wavulana 55 na wasichana 284 waliohitimu mafunzo ya kijeshi,ambapo watatakiwa kuendelea kuwepo katika kambi hiyo kujifunza stadi za maisha.
Aidha aliwataka vijana hao kuzingatia nidhamu waliyoelekezwa na wakufunzi wao na kuendelea kushiriki katika shughuli za maendeleo katika kambi hiyo kwa kuwa kambi hiyo inajishughulisha na shughuli za kilimo cha michikichi na alizeti kwa ajili ya kuwajenga vijana wanaoingia katika mafunzo kambini hapo kujiajiri wenyewe baada ya mafunzo.
Nae mwakilishi mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa Kanali Julius Kadawi alisema vijana wanatakiwa kuisaidia serikali katika masuala ya ulinzi na usalama na kuwa vielelezo kwa vijana wengine ambao bado hawajapata mafunzo hayo, kwa kuwa wakufunzi waliowafundisha vijana hao wamefanya kazi kubwa na kutokana na maonyesho walionesha yanaonesha jinsi gani walivyopikwa ipasavyo.
Na Rhoda Ezekiel - Malunde1 blog
ANGALIA PICHA HAPA CHINI
Mkuu wa wilaya ya Buhigwe Brigedia Jenerali Marko Gaguti akizungumza katika sherehe za kuhitimu mafunzo ya awali ya Kijeshi katika kambi hiyo wilayani Kigoma mkoani Kigoma- Picha na Rhoda Ezekiel - Malunde1 blog
Brigedia Jenerali Marko Gaguti akizungumza
Vijana waliohitimu mafunzo ya JKT wakimsikiliza Brigedia Jenerali Gaguti
Meza kuu wakifuatilia matukio wakati wa sherehe hizo