Rais wa awamu ya tatu wa Zimbabwe Emerson Mnangagwa anatarajia kuwasili nchini Tanzania kesho kwa ziara ya siku mbili kuanzia June 28 hadi 29 mwaka huu.
Akizungumza na vyombo vya habari leo jijini Dar es salaam Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Paul Makonda ameeleza kuwa Mnangagwa atapokelewa katika uwanja wa kimataifa wa mwalimu Nyerere na mwenyeji wake Rais John Magufuli majira ya saa tano kamili asubuhi.
Aidha ameeleza kuwa ujio huo wa Rais wa Zimbabwe una lengo kuu ambalo ni kudumumisha ushirikiano wa muda mrefu uliopo baina ya Tanzania na Zimbabwe tangu wakati wa kupigania uhuru wa taifa hili la kusini mwa Afrika.
Makonda amesema kwamba Mnangagwa ataondoka nchini June 29 asubuhi akisindikizwa na mwenyeji wake Rais Magufuli na ametoa wito kwa wakazi wa Dar es salaam kumkaribisha mgeni na wageni wote waingiao nchini kwa kuwafanya wajisikie wako nyumbani kwa muda wote watakaokuwa jijini.
Ikumbukwe kuwa hii ni ziara ya kwanza ya Rais Mnangagwa wa Zimbabwe kufika nchini Tanzania tangu alipoingia madarakani Novemba 2017.