Msanii wa Bongo Fleva aliyetamba na vibao kadhaa ikiwemo ‘sina raha’ na ‘hata kwetu wapo’ Sam wa Ukweli amefariki dunia usiku wa kuamkia leo katika Hospitali ya Palestina Sinza jijini Dar es salaam alipokuwa amelazwa kwa ajili ya matibabu.
Meneja na msambazaji wa nyimbo Amri the Business amesema kuwa Sam wa Ukweli amefariki majira ya saa nane usiku wa leo Alhamisi tarehe 7 Juni 2018 ambapo ni muda mfupi tu baada ya kufikishwa hospitalini hapo ambapo alikuwa anasumbuliwa na Malaria kwa muda wa wiki mbili.
Akizungumzia taarifa zilizosambaa mitandaoni kuwa marehemu alidai anaumwa ‘UKIMWI’ wa kurogwa amesema kuwa hafahamu chochote kuhusiana na taarifa hizo na ameishi na Sam kwa kipindi chote hakuwahi mshirikisha jambo hilo.
“Nimeishi na Sam kwa muda mrefu ameugua nilikuwa na taarifa za ugonjwa wake ndani ya wiki mbili lakini kuhusu suala hilo limekuwa geni na bado sijaelewa kwanini aliyezungumza kwanini amesema vile”, amesema Amri.
Amri ameongeza kuwa familia ya marehemu inaendelea na taratibu za mazishi pindi zitakapo kamilika wataweka wazi lakini taarifa za awali ni kwamba mwili utasafirishwa kupelekwa Bagamoyo kwa maziko.
Social Plugin