MAPACHA WA KIPEKEE TANZANIA WALIOUNGANA WAFARIKI DUNIA.....RAIS MAGUFULI AWALILIA


Maria na Consolata Mwakikuti enzi za uhai wao


Mapacha wa kipekee wa Tanzania walioungana, Maria na Consolata Mwakikuti wamefariki dunia usiku wa leo (Jumamosi, June 2) katika hospitali ya mkoa ya Iringa.

Taarifa zilizothibitishwa na mkuu wa wilaya wa Iringa Richard Kasesela, zimebainisha kuwa mapacha hao wamefariki wakipishana kwa takribani saa 2.

"Wamepigania sana afya zao, mida ya saa moja hivi jioni ndio nimepokea taarifa za kifo chao na kwa sababu nilikuwa mazingira ya hospitali basi nilisogea kuwaona – na ni kweli hatunao,” amesema Kasesela.

Taarifa kutoka hospitali inaonyesha pacha wa kwanza alifariki majira ya saa 1 usiku, huku mwenzake akifariki saa 3 usiku.

"Kwa hiyo taarifa zaidi na nini kinaendelea kesho tutakipata. Mungu awapumzishe pema peponi, Amina.”


Kufuatia vifo hivyo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli ametuma salamu za rambirambi kwa familia, Masista wa Maria Consolata na wote walioguswa na kifo cha mabinti mapacha walioungana Maria na Consolata Mwakikuti waliofariki dunia leo jioni katika hospitali ya Mkoa wa Iringa.

Mhe. Rais Magufuli aliwatembelea Maria na Consolata walipokuwa wakipata matibabu katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete Jijini Dar es salaam tarehe 06 Januari, 2018.

Pamoja na kuwapa pole, Maria na Consolata waliongoza sala ya kuliombea Taifa na Viongozi wake.

Mhe. Rais Magufuli anasema anatambua kuwa Maria na Consolata walikuwa na ndoto kubwa ya kuja kulitumikia Taifa baada ya kumaliza Chuo Kikuu cha Masista wa Consolata Ruaha (RUCO) walikokuwa wakiendelea na masomo yao, lakini haikuwa hivyo.


Amewaombea Mwenyezi Mungu aziweke roho zao mahali pema peponi, Amina.

Mapacha hao wamekuwa na historia ya matatizo ya moyo. Tangu Disemba 2017 pacha hao walianza kuumwa na kulazwa hospitali ya mkoa ya Iringa.

Baadaye walihamishiwa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKIC) katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, walipolazwa kwa takribani miezi miwili kwa ajili ya matibabu mpaka waliporuhusiwa kurejea tena Iringa mnamo Mei 17.

Maria na Consolata walizaliwa wilayani Makete mkoani Njombe mwaka 1996.

Walihitimu darasa la saba katika shule ya msingi Ikonda, kisha wakajiunga na shule ya Maria Consolata iliyopo Kilolo mkoani Iringa ambapo walihitimu kidato cha nne.

Baada ya hapo, walijiunga na shule ya Sekondari ya Udzungwa wilani Kilolo walipohitimu kidato cha sita, ikifuatiwa na Chuo Kikuu cha Katoliki cha Ruaha (Rucu) walipokuwa wakisomea fani ya ualimu.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post