Mwenyekiti wa kamati ya kuisaidia klabu ya Yanga Tarimba Abbas
***
Mwenyekiti wa kamati ya kuisaidia klabu ya Yanga kuvuka katika kipindi hiki cha mpito, Abbas Tarimba amesema kuwa watani wao wa kihistoria Simba hawana uwezo wa kung’amua vipaji vipya katika Soka na kuvisajili.
Huo ni mfululizo wa kauli mbalimbali za viongozi wa klabu hiyo kuhusu namna ambavyo watani wao wanavyosajili wachezaji wenye majina makubwa ambao awali walikuwa wanawaniwa na klabu yao, ambapo Katibu Mkuu wa Yanga, Charles Boniface Mkwasa aliwahi kukaririwa akisema baadhi ya vilabu vya ligi kuu vinatumia listi ya wachezaji ambao wao wamewaorodhesha kuwahitaji kwa kupitia mlango wa uwani na kuwasajili.
“Simba wamekuwa wakisubiri sisi tutaje wachezaji ambao tunawahitaji kuwasajili ili wao waje na kuwasajili kupitia mlango wa uwani jambo ambalo mimi naliona ni kukosa watu wazuri wa kusaka vipaji “.Alisema Tarimba.
Tarimba ameyasema hayo baada ya watani wao kumsajili mshambuliaji wa Gor Mahia, Meddie Kagere ambaye awali Yanga ilihusishwa kutaka kumsajili ili kuimarisha kikosi chake kuelekea katika michuano ya kombe la Shirikisho la Afrika na msimu mpya wa Ligi Kuu.
Mchezaji huyo aliyesajiliwa na Simba aling’ara katika michuano ya SportPesa Super Cup akiwa na klabu ya Gor Mahia ambapo aliibuka mfungaji bora wa michuano hiyo na kuzivutia klabu kadhaa Tanzania zikiwemo Simba na Yanga.
Katika siku za hivi karibuni, Abbas Tarimba aliwahi kuzungumza kuwa yeye na kamati yake watakuwa wanafanya usajili wao kimyakimya ili kuwaficha watani wao wasiweze kujua ni wachezaji gani wamewasajili.
Chanzo-EATV
Chanzo-EATV
Social Plugin