Romelu Lukaku na Eden Hazard walifunga mabao mawili kila mmoja na kuimarisha uongozi wa Ubelgiji dhidi ya England katika Kundi G kwa ushindi wa 5-2 dhidi ya Tunisia leo Jumamosi.
Kundi hilo linalowajumuisha pia Panama ambao watakutana na England Nizhny Novgorod Jumapili.
Bao la tano la Ubelgiji lilifungwa na Michy Batshuayi.
Tunisia walifungiwa na Dylan Bronn na Wahbi Khazri.
Tunisia wanatarajia Panama wawashinde England ndipo waweze kusalia katika michuano hiyo.
Hilo lisipofanyika basi Afrika itasalia na mataifa mawili pekee katika michuano hiyo - Nigeria na Senegal.
Lukaku amfikia Ronaldo kwa mabao
Lukaku sasa ana mabao manne katika Kombe la Dunia, sawa na Cristiano Ronaldo wa Ureno katika kinyang'anyiro cha kushinda Kiatu cha Dhahabu.
hazard alikuwa amemkosoa mchezaji huyo mwenzake, waliyecheza pamoja Chelsea wakati mmoja, kwa kutoweka wakati wa kipindi cha kwanza mechi dhidi ya Panama.
Lakini leo alitamba mechi yote hadi alipoondolewa uwanjani na nafasi yake akaingia Marouane Fellaini dakika ya 59.
Alionekana kuumia kidogo lakini anatarajiwa kurejea mechi dhidi ya England ambayo huenda ikaamua nani atamaliza kileleni kundi hilo.
Baada ya mechi ya leo, Hazard amemsifu sana.
"Tumeshinda mechi hii, kwa hivyo tuna furaha sana," ameambia BBC.
"Tulicheza vyema na kufunga mabao matano. Tumefungwa mawili, lakini tunaweza kujiimarisha. Hata hivyo, sasa tuna siku nne za kupumzika na kisha tucheze na England kushindania atakayemaliza kileleni kwenye kundi.
"Ni rahisi sana kucheza na Lukaku, unampa mpira na anafunga kila wakati. Alicheza vizuri sana."
Tunisia hawana matumaini
Tunisia leo walicheza vyema na kushambulia zaidi ukilinganisha na mechi ya kwanza ambapo walishindwa na England, lakini walitatizika kufunga.
Carthage Eagles walishambulia goli mara 16, mara tano makombora yao yakilenga goli, ukilinganisha na mechi dhidi ya England waliposhambulia mara nne na walifanikiwa kulenga goli mara moja pekee.Bila shaka leo hakuna mchezaji wa Ubelgiji atamkosoa Lukaku kwa uchezaji wake
Ikizingatiwa kwamba England wanachezaji dhidi ya Panama Jumapili, labda lengo la Tunisia sasa litakuwa kujaribu kuzuia kumaliza wa mwisho katika kundi hilo kwa kumaliza nyuma ya Panama watakapokutana Alhamisi wiki ijayo.
'Tunawaomba radhi mashabiki wa Tunisia'CHRIS BRUNSKILL/FANTASISTA
Kocha wa Tunisia Nabil Maaloul amewaomba radhi mashabiki baada ya kushindwa leo.
"Kama tulivyotarajia, ilikuwa mechi ngumu sana."
"Tokea wakati tulipopangwa kwenye kundi hilo, tulijua Ubelgiji wangekuwa wapinzani hatari. Tungependa kuwaomba radhi mashabiki wa Tunisia waliojitokeza kwa wingi sana uwanjani leo.
"Hata hivyo, tulifanya kadiri ya uwezo wetu na tutajaribu kuboresha uchezaji wetu siku za usoni."
Takwimu: Lukaku amfikia Diego Maradona
- Ubelgiji wamefunga katika kila mechi kati ya sita walizocheza karibuni hatua ya makundi Kombe la Dunia - walishinda ya mwisho 2002, na zote tatu 2014 na pia wakashinda za kwanza mbili michuano ya sasa.
- Tunisia sasa hawajashinda hata mechi moja kati ya 13 walizocheza Kombe la Dunia (walitoka sare 4 na kushindwa 9) - wameshindwa mechi nne za karibuni zaidi mfululizo.
- Lukaku sasa amefunga mabao mengi michuano mikubwa ya kimataifa (Ubingwa Ulaya na Kombe la Dunia) kuliko mchezaji mwingine yeyote yule wa Ubelgiji (mabao saba).
- Lukaku amefunga mabao 17 katika mechi 11 alizochezea Ubelgiji karibuni zaidi, ni katika mechi moja pekee ambapo hakufunga (dhidi ya Ureno mapema mwezi huu).
- Ubelgiji wamefunga mabao matano katika michuano ya Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza katika historia sasa.
- Lukaku ndiye mchezaji wa kwanza kufunga mabao mawili au matatu katika michuano inayofuatana ya Kombe la Dunia tangu Diego Maradona alipofanya hivyo 1986, alifunga mabao mawili dhidi ya England na dhidi ya Ubelgiji.
- Penalti ya Hazard imekuwa bao la pili la kasi zaidi kwa Ubelgiji Kombe la Dunia (5:59), nyuma ya bao la Leopold Anoul dhidi ya England mwaka 1954 lililofungwa dakika ya tano.
- Ubelgiji wameshinda mechi 11 kati ya 12 za ushindani walizocheza dhidi ya Roberto Martinez, hiyo nyingine walitoka sare. Wamefunga mabao 51 na kufungwa manane pekee mechi hizo.
- Hazard sasa amechangia magoli 23 katika mechi 21 alizochezea Ubelgiji karibuni (amefunga 11, na kusaidia ufungaji wa 12).
Nini kinafuata?
Ubelgiji watakamilisha kampeni yao dhidi ya England uwanja wa Kaliningrad Alhamisi, siku ambayo Tunisia nao watakutana na Panama uwanja wa Mordovia Arena, Saransk (mechi zote zitaanza saa tatu usikusaa za Afrika Mashariki).