Wako watu wanaojiamini na wanajihisi wenye uwezo wa kujizuia, lakini mara wanapokuwa katika ulevi wowote ule hushindwa kujizuia. Hili lipo kwa wanawake na hata wanaume. Tabia ya ulevi wowote hupunguza uwezo wa mtu kufikiria ilivyo sahihi.
Unaweza kukuta watu wameketi pamoja na wanaheshimiana lakini kwa kadri wanavyoendelea kulewa wanaanza kushikana maungo na kila mmoja anaona ni sawa tu, heshima na nidhamu waliyokuwa nayo awali imeshapeperukia dirishani kwa sababu ya ushawishi wa ulevi.
Hali hii ina majuto sana maana mtu anajikuta kasha shiriki ngono na mtu mwingine, ama mtu anayemjua au hata asiyemjua pasipo utashi wake.
Majuto yanakuwa makubwa zaidi maana mara nyingine hata usiri unakuwa haupo, heshima na nidhamu yako yote inaathirika.
Zipo baadhi ya pombe ambazo badala tu ya kukuondolea aibu, zinaweza kukulegeza mwili na viungo na kuongeza hamu ya ngono. Ndio maana watu wanaotumia vilevi wanashauriwa kuwa na wenza wao katika nyakati hizi ili walao kujizuia kuingia mitegoni.
Watu wengi tuliowahoji nyakati za ushauri wanakiri kwamba safari ya kuingia kwenye mahusiano ya kingono na watu wa nje ilisindikizwa zaidi na matumizi ya kilevi au vilevi, na wengine wanaendelea kukiri kwamba ni ngumu kuchepuka bila kuwa na kilevi akilini.
Kutostahimili ukaribu usio na mipaka
Wapo watu wengi ambao wamejikuta wakikamatika katika mahusiano ya kingono na wale waliowaita marafiki wa karibu. Mwanzoni alionekana kama rafiki, mnashauriana, mnasaidiana, mnasindikizana, mnatembeleana, na wala haukuwahi kudhani mngefikia hapo mlipofikia.
Lakini kwa sababu mlishindwa kuwa makini kwenye kuilinda mipaka ya urafiki wenu, sasa uhusiano wa kawaida na wa urafiki umekuwa uhusiano wa kingono.
Hali hii huathiri uthamani wa urafiki baina ya watu na mara nyingine waliokuwa marafiki wanaweza kuja kuwa maadui kabisa. Ukaribu zaidi na mtu wa jinsia ya tofauti na wewe huwa sio mzuri sana kwa afya ya mahusiano au ndoa yenu.
Yamkini unajitetea kwamba hakuna kinachoweza kutokea lakini fahamu kwamba hata kikija kutokea hautakuwa na ujasiri wa kusema kwamba kuna kilichotokea. Heri kuziba ufa kuliko kujenga ukuta.
Ninakushauri kwamba watu wote ambao uko nao karibu ni vema wafahamike kwa mwenza wako, epuka urafiki wa sirini, na mikutano ya sirini.
Mkutano na rafiki ambaye uko naye karibu na wa jinsia tofauti kamwe usifanyike maeneo ya kificho au sehemu ambayo mko peke yenu.
Yamkini nia na dhumuni lenu sio ovu lakini mazingira shawishi yanaweza kuwafikisha ambako hamkupanga kufika.
Kuwa na ujasiri wa kuiweka mipaka ya urafiki wenu bayana, na rafiki yako au rafiki zako waiheshimu mipaka yako. Iheshimu mipaka hiyo maana usipoiheshimu mipaka yako na wengine kamwe hawawezi kuiheshimu mipaka hiyo. Pia ukitaka watu waheshimu mipaka yako na wewe pia iheshimu mipaka ya wengine. Na mwisho ni kwamba kamwe usimwamini yeyote kwa asilimia 100, Jilinde uwapo mazingira yeyote.
Kulipiza kisasi
Aina hii ya kuchepuka huwa kwa wanaume na wanawake ingawa inaripotiwa zaidi kuonekana kwa wanaume kwa sababu ya ukweli kwamba mara nyingi wanaume wanaweza wakakwazika na bado wasifunguke kuelezea walivyokwazwa lakini wakati huohuo wana kiu ya kulipiza kisasi kwa maumivu waliyoyapata tofauti na wanawake ambao wao kufunguka ni rahisi na ni kawaida kwao.
Wanaume kwa kawaida wanaweza kuamua kutoka nje ya ndoa kwa sababu tu amekasirishwa na kuona haheshimiwi katika mambo fulani kwenye mahusiano au familia.
Kwa mfano akihisi hasikilizwi, hapewi kipaumbele, hahudumiwi, anachosema hakifuatwi anavyotamani havifanywi basi kuna uwezekano mkubwa akaanzisha mahusiano pembeni kwa siri.
Tafiti za kisaikolojia zinasema kwamba mwanaume anapochepuka kwa msukumo wa hali kama hizi ile hali ya kujihisi anafanya kosa inapungua au kupotea kabisa na kwahivyo anaweza kujihesabia haki kabisa kwa kile anachokifanya.
Hii inaweza kumfanya aendelee kuchepuka kwa muda mrefu zaidi tofauti na mwanamke ambaye hata hali hii ikijitokeza wengi huwa wanajihisi kuhukumiwa na kujisikia vibaya moyoni.
Kuchepuka kwa kulipiza kisasi hutokea pia nyakati ambazo mwanandoa mmoja anahisi kuwa mwenzake ana mahusiano nje, iwe kuna ushahidi au ni tetesi, wengine jambo hili humsukuma na yeye kufanya hivyohivyo ili kutafuta uwiano au kujisuuza nafsi.
Kwa bahati mbaya matokeo ya tabia hizi yamekuwa hasi zaidi na kwa wengi imepelekea kuharibu mahusiano na ndoa.
Ninashauri kwamba yanapotokea maumivu au makwazo ya aina yeyote yasihifadhiwe moyoni au kuonewa aibu kuzungumzwa maana visasi havilipi bali huongeza maumivu na uharibifu zaidi.
Social Plugin