Mwakilishi wa Katibu Tawala Mkoa wa Dodoma Bi. Honoratha Rwegasira akitoa hotuba ufunguzi kwa niaba ya Mgeni rasmi wakati wa Kongomano la Wajane lililofanyika Jijini Dodoma.
Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na Umoja wa Mataifa unaonesha kuwa kati ya asilimia 7 na 16 ya wanawake wote duniani ni Wajane ambapo Takwimu zinakadiria kuwa duniani kuna wajane milioni 285 na kati yao hao milioni 115 hali zao kiuchumi ni mbaya.
Jamii imetakiwa kuendeleza mipango na kuongeza juhudi zaidi katika kukabiliana na vitendo vya ukatili, unyanyasaji na kuwainua wajane ili wapate uwezo wa kiuchumi wa kuzihudumia familia na wategemezi wao kwa kuwa ndiyo muhimili pekee wa familia iliyoachwa.
Akiongea kwa niaba ya Mgeni rasmi wa kongamano la Wajane liliofanyika katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mwakilishi wa Katibu Tawala Mkoa Bi. Honoratha Rwegasira amepongeza juhudi za wadau wa maendeleo na serikali katika kuwasaidia wajane kuleta usawa wa kinjisia na kuinua ushiriki wao katika ngazi za kutoa maamuzi.
Aidha Bi. Rwegasira ameitaka jamii kuacha mila potofu kama vile kunyanganya mali mjane, kuozesha watoto wa kike katika umri mdogo, kurithi wajane na nyingine zote zinazoweza kumdhoofisha mwanamke katika jitihada zake za kujikwamua kifikra, kiutamaduni, kiuchumi,kijamii na kisiasa.
Wakati huo huo Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Jinsia kutoka Wizara ya Afya,Idara Kuu Maendeleo ya Jamii Bi. Mwajuma Magwiza amesema kimsingi lengo la maadhimisho ya Siku ya Wajane Duniani ni kutoa nafasi kwa Wadau kushirikiana na Serikali kwa kutoa huduma za msingi kwa wajane na kuondoa aina zote za ukandamizaji ikiwemo haki ya kumiliki mali, umasikini, mira na desturi za kurithiwa baada ya kufiwa.
Chanzo- EATV