Wezi ambao hawajafahamika idadi wala majina mpaka sasa juzi waliingia nyumbani kwa mchungaji wa Kanisa la TAG mkoani Morogoro, Jastine Dume 'Muro' kisha kumnyonga hadi kufa mfanyakazi wake wa ndani.
Wezi hao walimnyonga mfanyakazi huyo, Habiba Rashidi (21) kwa kutumia kamba ambayo waliitundika katika chumba anacholala msichana huyo.
Kaimu Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Morogoro, Kamishna Msaidizi wa Polisi, Mugabo Wekwe, alisema jana kuwa tukio hilo lilitokea Jumanne, Kihonda Uwanja wa Ndege mkoani humo.
Kamishna Wakwe alisema baada ya kufanya mauaji hayo, wezi hao waliiba vitu mbalimbali na Sh. 200,000.
Alisema juhudi za kuwasaka wauaji hao zinaendelea kufanyika.
Alitaja vitu vilivyoibiwa kuwa ni redio ndogo nne, simu, deki ya TV na Sh. 200,000 taslimu.
Wakati huo huo, Kamanda Wekwe alisema uchunguzi dhidi ya tukio la Amina Rafael mkazi wa kijiji cha Mgudeni, Kilombero ambaye inadaiwa amejifungulia nje ya kituo cha polisi baada ya kutolewa maabusu, umefikia hatua za mwisho.
"Tupo katika hatua za mwisho za uchunguzi wa tukio hili (na) tutatoa taarifa kamili wakati wowote," alisema, "changamoto ni kwamba kituo cha polisi kinachodaiwa kufanyika tukio hili kipo mbali hivyo tume inaendelea kukamilisha uchunguzi wake."
Taarifa za awali zilidai Amina alipokuwa mahabusu kwa kosa la mumewe alilalamika kuumwa uchungu lakini askari wa zamu alipuuza hadi alipoona amezidiwa na kumtoa nje.
Taarifa hizo zinadai kuwa baada ya mwanamke huyo kutolewa nje alijifungulia kwenye nyasi bila ya msaada na baadaye kupelekwa kituo cha afya cha Mang'ula.