SERIKALI inakusudia kutunga sheria itakayowabana vijana ambao wamekuwa na tabia ya kutelekeza na kutowatunza wazazi wao.
Hayo yalibainishwa juzi na Kamishna wa Ustawi wa jamii Naftali Ng’ondi, wakati alipokuwa akifungua maadhimisho ya siku ya kuelimisha na kupinga vitendo vya ukatili kwa wazee iliyofanyika jijini hapa.
Alisema kuwa vijana wengi wamekuwa na tabia ya kutelekeza wazee wao na kuiachia mzigo serikali hali ambayo itakomeshwa kupitia sheria hiyo itakayotungwa.
“Vijana wamekuwa wakitelekeza wazazi wao pindi wanapofikia hali ya uzee na kutokana na hali hii serikali kwa kushirikiana na wadau wengine itatunga sheria itakayowabana,”.
“Kuna baadhi ya nchi tayari wameshaanza lakini na sisi tunahitaji kuwa nayo ili kupunguza hali hii kama leo mzazi akitelekeza mtoto sheria inachukuliwa basi na kwa hawa vijana iwe hivyo hivyo”alisema.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Shirika linalojihusisha masuala ya wazee la Help Age, Smart Daniel alisema njia mojawapo ya kuwasaidia wazee ni kuhakikisha serikali inaanza kutekeleza mpango wa kutoa pensheni kwa kundi hilo.
Alisema suala la pensheni kwa wazee ni jambo ambalo halikwepeki hata kidogo kutokana na umuhimu wa kundi hilo ambalo lilijitolea katika kulipigania Taifa.
“Sisi tulikuwa wa kwanza katika kupigania suala la pensheni kwa wazee, lakini wenzetu wa visiwani Zanzibar wakalichukua suala hili na leo hii kwao ni mwaka wa tatu wanatoa pensheni kwa wazee wao,” alisema.
Danieli, aliongeza kuwa katika ukanda huu wa nchi za jumuiya ya Afrika Mashariki pia nchi ya Kenya imekuwa ya pili kuanza kutoa pensheni ya wazee wenye umri wa kuanzia miaka 70.
“Sasa kama Zanzibar wamechukua nafasi ya kwanza na Kenya ya pili basi sisi Tanzania bara hii nafasi ya tatu tusipoteze kwani tunatakiwa kuanza kutoa pensheni kwa wazee wetu,”alisema Danieli.
Mmoja wa wazee kutoka mkoani Simiyu, Clotilda Kokupima, alisema wazee bado wanahitaji sana pensheni kutokana na hali za kimaisha walizo nazo.
“Wazee tunapata tabu sana wengi wetu tunadhulumiwa, tunapingwa lakini kama suala la kuwalinda wazee litawekewa sheria kali pamoja na kuanza kupatiwa pensheni basi tutakuwa tumesaidiwa sana,”alisema Kokupima.
Chanzo- NIPASHE