Picha : NAIBU WAZIRI WA AFYA AIPONGEZA AGPAHI KWA KUIMARISHA HUDUMA ZA TIBA NA MATUNZO KWA WATU WANAOISHI NA VVU


Kulia ni Mkurugenzi Mtendaji wa AGPAHI, Dkt. Sekela Mwakyusa akikabidhi Televisheni kwa Naibu Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto, Dkt. Faustine Ndugulile kwa ajili ya klabu ya watoto katika kituo cha tiba na matunzo (CTC) cha hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Mara.

***

Naibu Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto, Dkt. Faustine Ndugulile ameipongeza asasi ya kitaifa isiyo ya kiserikali ya Ariel Glaser Pediatric AIDS Healthcare Initiative (AGPAHI) kwa kuimarisha huduma za tiba na matunzo kwa watu wanaoishi na VVU mkoani Mara. 

Dkt. Ndugulile alitoa pongezi hizo Julai 19,2018 wakati akiwa katika katika ziara ya kikazi mkoani Mara na kushuhudia kazi zinazofanywa na AGPAHI katika hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Mara katika kuhudumia watu wanaoishi na VVU ambapo pia alipokea vifaa vya michezo vilivyotolewa na AGPAHI kwa ajili ya klabu ya watoto iliyopo katika hospitali hiyo. 

"Nimekuja kupata ushuhuda wa kazi kubwa ambayo wadau wetu wa maendeleo AGPAHI wanafanya katika kudhibiti maambukizi ya Ukimwi,niwashukuru na kuwapongeza kwa kazi kubwa mnayofanya kwa kushirikiana na serikali katika kudhibiti ugonjwa wa UKIMWI, na tunawashukuru kwa misaada mbalimbali mnayotupatia”,alisema Dkt. Ndugulile. 

"Serikali inafarijika sana kuona wadau wanakuwa na mchango mkubwa katika kudhibiti UKIMWI, kama wadau wa maendeleo tunatarajia wataziba mapengo pale serikali haijafika kinachotakiwa ni kushirikiana, tunataka NGO's zote zinazofanya kazi katika mkoa wa Mara ziendane na vipaumbele vya mkoa”,aliongeza. 

Aidha Dkt. Ndugulile alisema serikali imedhamiria kuhakikisha kuwa ifikapo mwaka 2020 asilimia 90% ya watu wenye maambukizi ya VVU wanafikiwa na kupimwa,ambapo asilimia 90% ya walioathirika wanapewa dawa za kufubaza virusi na asilimia 90% ya watakaotumia dawa hizo hawataweza kuwaambukiza watu wengine kwa sababu virusi vitakuwa vimefubazwa na tiba hiyo. 

“Mpaka sasa tumewafikia Watanzania takribani milioni 1.4 wanaohisiwa kuwa wanaishi na VVU, bado tunapambana kuwafikia laki nne ambao hatujawafikia, lakini sambamba na hayo tunaendelea kupambana kuhakikisha maambukizi mapya tunayadhibiti kwa kuweka mikakati mbalimbali ikiwemo kudhibiti maambukizi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto”,alisema. 

Alisema serikali itaendelea kuhakikisha kuwa dawa za kufubaza makali ya VVU zinaendelea kupatikana kwa asilimia 100 huku akiwasisitiza wanaume kujitokeza kupima afya zao ili kubaini kama wana maambukizi ya VVU na wakibainika wameambukizwa basi waanze kutumia dawa za kufubaza makali ya VVU. 

Akitoa taarifa ya kazi zinazofanywa na AGPAHI, Mkurugenzi Mtendaji wa AGPAHI, Dkt. Sekela Mwakyusa alisema katika mkoa wa Mara,wanatoa huduma katika vituo 113 vya kutolea huduma za afya,68 vya huduma ya matunzo na matibabu kwa watu wanaoishi na VVU (CTC) na vingine 45 vya kuzuia maambukizi ya VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto (PMTCT). 

“Tunatekeleza mradi wa Boresha kwa ufadhili wa serikali ya Marekani kupitia shirika la Centres for Disease Control (CDC),ambapo mradi huu unatoa huduma za kinga,tiba na matunzo kwa watu wanaoishi na VVU”,alisema. 

Dkt. Sekela alibainisha kuwa kuanzia mwezi Oktoba 2017 hadi Machi 2018,AGPAHI imefanikiwa kupima watu 162,389 ambapo kati yao 4,482 sawa na asilimia 2.7 waligundulika kuwa na maambukizi ya VVU wakiwemo watoto 265. 

“Katika kipindi hicho pia watoto 988 walizaliwa na akina mama wenye VVU lakini kutokana na huduma za kukinga watoto dhidi ya maambukizi kutoka kwa mama, watoto 934 sawa na 98% hawakuwa na maambukizi, na 16 waliopata maambukizi wanaendelea kupata huduma za VVU”,alieleza Dkt. Sekela. 

“AGPAHI ilipoanza kutekeleza mradi wa Boresha hapa Mara Oktoba 2016 kulikuwa na watu 25,821 wanaopata huduma za VVU na UKIMWI,lakini kwa kushirikiana na serikali tumeweza kuwafikia watu 31,729 ‘wanaume 9,202 (29%),wanawake 22,527 na watoto 1,664,tunaendelea na upimaji hasa tukilenga kuwatambua wanaume wenye maambukizi ili waanze kupata huduma hizi muhimu”,alifafanua Dkt. Sekela. 

Aidha aliongeza kuwa katika kuunga mkono juhudi za serikali za kupambana na upungufu wa wafanya kazi kwa kada ya afya,AGPAHI imewezesha ajira kwa watumishi wapatao 201 kati yao 118 ni makarani takwimu na 83 ni maafisa tabibu,wataalam wa maabara na wauguzi. 

Dkt. Sekela alisema mbali na kuwajengea uwezo Washauri wa Watu Wanaoishi na VVU 123 na kuanzisha vikundi vya WAVIU pia AGPAHI inaendelea kutoa misaada mbalimbali ikiwemo vifaa vya michezo,televisheni na kutengeneza vifaa vya michezo. 

“Kupitia mradi wa Boresha AGPAHI imetoa kompyuta 86 kwa ajili ya kurahisisha mfumo wa takwimu katika halmashauri zote za mkoa wa Mara,tumetoa Cryotherapy mashines kwa ajili ya matibabu ya dalili za mwanzo za saratani ya mlango wa kizazi,solar panels kwenye vituo vya afya,kuboresha vituo vya afya,majokofu ya kutunzia dawa,darubini na vitu mbalimbali”,aliongeza. 


Ariel Glaser Pediatric AIDS Healthcare Initiative (AGPAHI) ni asasi ya kitaifa isiyo ya kiserikali iliyoanza kushirikiana na serikali ya Tanzania katika juhudi za kutokomeza VVU na UKIMWI kwa watoto tangu 2011 katika mikoa ya Shinyanga na Simiyu kisha Mwanza,Geita,Mara na Tanga kwa ufadhili wa Serikali ya Marekani kupitia vituo vya Kudhibiti Magonjwa na Kinga (CDC). 

ANGALIA MATUKIO KATIKA PICHA
Wa pili kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa AGPAHI, Dkt. Sekela Mwakyusa akiteta jambo na Naibu Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto, Dkt. Faustine Ndugulile wakati wakielekea katika kituo cha tiba na matunzo (CTC) cha hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Mara kwa ajili ya kushuhudia kazi zinazofanywa na AGPAHI katika kuimarisha huduma za tiba na matunzo kwa watu wanaoishi na VVU.Kushoto ni Afisa Miradi Huduma Unganishi kwa Jamii AGPAHI mkoa wa Mara, Alio Hussein.- Picha zote na Kadama Malunde - Malunde1 blog
Naibu Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto, Dkt. Faustine Ndugulile akielekea katika kituo cha tiba na matunzo (CTC) cha hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Mara.
Kulia ni Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Mara,Dkt. Joachim Eyembe akitoa taarifa kuhusu huduma za afya katika hospitali hiyo kwa Naibu Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto, Dkt. Faustine Ndugulile.
Naibu Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto, Dkt. Faustine Ndugulile akizungumza katika hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Mara na kuupongeza uongozi wa hospitali hiyo kwa kuimarisha huduma za afya na kupunguza malalamiko kutoka kwa wagonjwa.
Naibu Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto, Dkt. Faustine Ndugulile akizungumza katika hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Mara.
Mkurugenzi Mtendaji wa AGPAHI, Dkt. Sekela Mwakyusa akitoa taarifa ya kazi zinazofanywa na AGPAHI katika kuimarisha huduma za tiba za matunzo kwa watu wanaoishi na Virusi Vya UKIMWI mkoani Mara. Kushoto ni Mbunge wa Jimbo la Musoma Mjini, Vedastus Manyinyi Mathayo.
Mkurugenzi Mtendaji wa AGPAHI, Dkt. Sekela Mwakyusa akifafanua kuhusu huduma mbalimbali zinazotolewa na AGPAHI mkoani Mara.
Mkurugenzi Mtendaji wa AGPAHI, Dkt. Sekela Mwakyusa akiwasisitiza viongozi wa serikali kuendelea kushirikiana na AGPAHI katika kudhibiti maambukizi ya VVU.
Mkurugenzi Mtendaji wa AGPAHI, Dkt. Sekela Mwakyusa akiishukuru serikali kwa kuwapa fursa ya kuwatumikia Watanzania kuleta mabadiliko chanya kwenye masuala ya afya hasa UKIMWI.
Vifaa vilivyotolewa na AGPAHI kwa ajili ya klabu ya watoto na vijana wa kituo cha tiba na matunzo katika hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Mara.Vifaa hivyo ni televisheni,mipira,mikeka,viti na vitabu.
Viongozi mbalimbali akiwemo Naibu Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto, Dkt. Faustine Ndugulile,Mbunge wa Jimbo la Musoma Mjini, Vedastus Manyinyi Mathayo,Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Mara,Dkt. Joachim Eyembe na Mkuu wa wilaya ya Musoma, Dkt. Vicent Anney wakiangalia vifaa vilivyotolewa na AGPAHI kwa ajili ya klabu ya watoto na vijana katika kituo cha tiba na matunzo cha hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Mara.
Kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa AGPAHI, Dkt. Sekela Mwakyusa akielezea kuhusu vifaa hivyo ambavyo ni pamoja na vifaa vya michezo.Alisema mbali na kutoa vifaa vya michezo pia wameboresha viwanja vya michezo katika hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Mara.
Kulia ni Mkurugenzi Mtendaji wa AGPAHI, Dkt. Sekela Mwakyusa akikabidhi Televisheni kwa Naibu Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto, Dkt. Faustine Ndugulile kwa ajili ya klabu ya watoto katika kituo cha tiba na matunzo (CTC) cha hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Mara.
Kulia ni Mkurugenzi Mtendaji wa AGPAHI, Dkt. Sekela Mwakyusa akikabidhi Televisheni kwa Naibu Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto, Dkt. Faustine Ndugulile kwa ajili ya klabu ya watoto katika kituo cha tiba na matunzo (CTC) cha hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Mara.
Kushoto ni Naibu Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto, Dkt. Faustine Ndugulile akikabidhi televisheni kwa Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Mara,Dkt. Joachim Eyembe kwa ajili ya klabu ya watoto katika kituo cha tiba na matunzo (CTC) cha hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Mara.
Naibu Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto, Dkt. Faustine Ndugulile akikabidhi vitabu kwa mmoja wa vijana kutoka klabu ya vijana katika CTC ya hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Mara.
Kijana akiishukuru AGPAHI kwa kuwapatia vifaa vya michezo.
Vijana kutoka CTC ya hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Mara wakionesha igizo linalotoa elimu kuhusu umuhimu wa kuwa wafuasi wazuri wa dawa za kufubaza makali ya VVU.
Wafanyakazi wa hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mara wakifuatilia igizo.
Mshauri wa Watu Wanaoishi na VVU Nehemia Kaswala Mtumi anayeishi na maambukizi ya VVU tangu mwaka 1995 na mke mmoja na watoto watano wote hawana maambukizi ya VVU akielezea namna wanavyoshirikiana na AGPAHI na serikali katika kuhamasisha masuala ya afya kwa watu wanaoishi na VVU,uzazi wa mpango,TB na uchunguzi wa saratani ya shingo ya mlango wa kizazi,upimaji wa VVU nyumba kwa nyumba na uundaji wa vikundi vya WAVIU.
Naibu Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto, Dkt. Faustine Ndugulile akiandika dondoo muhimu wakati Mshauri wa Watu Wanaoishi na VVU Nehemia Kaswala Mtumi akitoa salamu za WAVIU Washauri kutoka hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Mara.
Kulia ni Mkuu wa wilaya ya Musoma, Dkt. Vicent Anney akimweleza jambo Mkurugenzi Mtendaji wa AGPAHI, Dkt. Sekela Mwakyusa.
Mkurugenzi Mtendaji wa AGPAHI, Dkt. Sekela Mwakyusa na Naibu Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto, Dkt. Faustine Ndugulile wakifurahia jambo.
Mshauri wa Watu Wanaoishi na VVU Nehemia Kaswala Mtumi akikabidhi taarifa yake kwa Naibu Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto, Dkt. Faustine Ndugulile.
Kijana akisoma risala kuhusu klabu ya watoto kutoka Kituo cha tiba na Matunzo (CTC) cha hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mara.Alisema tangu AGPAHI ianze kufadhili klabu hiyo mwaka 2017 wamefanikiwa kuongeza uelewa kuhusu VVU,UKIMWI, lishe bora,umuhimu wa mazoezi na ufuasi mzuri wa dawa. Aidha aliitaka serikali na wadau kuielimisha jamii kuacha unyanyapaa kwa watu wanaoishi na VVU kwani wanahitaji upendo badala ya unyanyapaa.
Naibu Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto, Dkt. Faustine Ndugulile akizungumza kwenye kituo cha tiba na matunzo (CTC) katika hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mara. Aliwataka watu wanaoishi na maambukizi ya VVU kuwa wafuasi wazuri wa dawa na wale ambao ambao hajapima afya hususani wanaume kujitokeza kupima ili wajue hali ya afya zao.
Naibu Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto, Dkt. Faustine Ndugulile pia aliitaka jamii kuacha tabia ya kunyanyapaa watu waliopata maambukizi ya VVU na kusisitiza kuwa dawa za kufubaza makali ya VVU zipo za kutosha.
Kushoto ni Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mara Dkt. Francis Mwanisi akiteta jambo na Naibu Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto, Dkt. Faustine Ndugulile. 
Vijana kutoka CTC ya hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Mara wakicheza mchezo wa kuchangamsha akili na mwili 'Chicken Dance'. 
Naibu Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto, Dkt. Faustine Ndugulile akicheza na watoto mchezo wa kuchangamsha akili na mwili 'Chicken Dance'. 
Mchezo wa kuchangamsha akili na mwili 'Chicken Dance' ukiendelea. 
Wafanyakazi wa AGPAHI wakiwa katika picha ya pamoja.

Picha zote na Kadama Malunde - Malunde1 blog

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post