Christopher Williams Jr.
Mtoto wa umri wa miaka miwili nchini Marekani amefariki baada ya kujipiga risasi kichwani kwa bunduki ambayo imekuwa ikihifadhiwa na wazazi wake nyumbani kwao.
Polisi wa Houston, Texas wanasema wazazi wa mtoto huyo - Christopher Williams Jr - walikuwa nyumbani wakati wa kutokea kwa kisa hicho.
Polisi wanasema bunduki hiyo ambayo hutumia risasi za ukubwa wa 9mm ilipatikana eneo la tukio na kwamba ilikuwa inamilikiwa na babake.
Kufikia sasa, bado haijabainika iwapo wazazi wake watashtakiwa.
Watoto kadha wamekuwa wakijipiga risasi na kujiua kimakosa nchini Marekani miaka ya karibuni.
Polisi wa Houston wamesema wanajaribu kubaini ni vipi mtoto huyo aliyepewa jina la utani "Junior" aliweza kuifikia bunduki hiyo.
Mkuu wa kitengo cha waathiriwa maalum katika idara ya polisi ya Houston David Angelo ametoa wito kwa wazazi walio na bunduki kuchukua tahadhari zaidi.
"Ni lazima uweke salama silaha, iwe ni kwa kuhakikisha kifaa cha kufyatulia risasi kimewekwa salama au kuiweka salama silaha kwa njia nyingine kuhakikisha matukio kama haya hayatokei tena siku za usoni," alisema.
Alieleza kisa hicho kuwa cha kusikitisha sana.
Binamu yake marehemu Suzzane Alvarado ameambia ABC 13 kwamba marehemu "hakustahili yaliyomkuta. Alikuwa mtoto mdogo na mwenye matumaini makubwa maishani."
Kwa mujibu wa gazeti la Houston Chronicle, babake marehemu Christopher Charles Williams, alipatikana na hatia ya kuwa na bastola kinyume cha sheria mwaka 2009.Haki miliki ya pichaFAMILY HANDOUT/ KHOUImage caption
Bi Alvarado alimweleza kama baba mwenye kuwajibika sana kwa mwanawe.
"Saa 24 kwa siku, alikuwa na mwanawe. Alikuwa akifanya zaidi ya kina baba wengine."
Jumatatu, polisi Houston walimshtaki baba mwingine kutokana na kujipiga risasi kimakosa kwa mwanawe wa kiume mwezi Mei.
Ali Parvez Masoom, 32, anadaiwa kuiacha bunduki yake aina ya .308 mezani ambapo mwanawe aliweza kuifikia na kujipiga risasi usoni.
Bw Massom aliachuliwa huru baada ya kulipa dhamana ya $1,000 (£750) na kwa sasa anakabiliwa na kosa la kutowajibika na kumuwezesha mtoto kuifikia silaha.
Jumamosi, mtoto mwingine wa miaka miwili alifariki Fresno, California katika kisa karibu sawa na hicho.
Wazazi wa mtoto huyo walikuwa nyumbani alipoifikia bastola hiyo na kujipiga risasi kichwani.
Chanzo - BBC
Social Plugin