AUAWA AKIOMBWA MOTO WA KUWASHIA SIGARA


Watu wawili wameuawa katika matukio mawili tofauti likiwamo la Richard Kishaju (49), mkazi wa Mtaa wa Manga wilaya na mkoa wa Geita kutenganishwa kiganja cha mkono wa kushoto na kiwiliwili na wauaji waliokuwa wamemuomba moto wa kuwashia sigara.


Katika tukio jingine, Didi Aroon (47) mkazi wa Kijiji cha Kasesa wilayani Geita anashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma za kumuua mwanaye kwa kumcharaza viboko kwa madai ya kuchukizwa kwenda kutembea kwa jirani.

Akithibitisha jana kutokea kwa matukio hayo, Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Geita, Mponjoli Lotson alisema Kishaju aliuawa baada ya kuvamiwa na watu watatu wasiojulikana.

Alisema watu hao walimshambulia kwa mapanga sehemu kadhaa za mwili na kisha kutokomea.

Kamanda Mpojoli alisema wauaji hao walifika nyumbani kwa marehemu saa mbili usiku Juni 27 na kisha kuomba moto wa kuwashia sigara, lakini wakiwa katika hatua hiyo ndipo mmoja alipochomoa panga na kuanza kumkatakata marehemu.

"Watuhumiwa bila huruma walimkatakata na kisha kutengenisha kiganja chake cha mkono wa kushoto kwa kuanguka chini kisha kutokomea," alisema na kueleza kuwa uchunguzi wa tukio hilo umeanza.

Kamanda Mponjoli alisema katika tukio lingine, Aroon anadaiwa kumuua mwanaye Sele Didi mwenye umri wa miaka 10 kwa kipigo.

Mtoto huyo alikuwa akisoma darasa la pili katika Shule ya Msingi Kasesa.

Kamanda Mpojoli alisema mtuhumiwa anashikiliwa na polisi na kueleza kuwa chanzo cha kumpiga, ni baba huyo kuchukizwa na mwanawe kwenda kutembea kwa jirani.

Kamanda huyo pia alitaka jamii kuchukua tahadhari pale wanapoona watu wasiowafahamu wakijaribu kujenga mahusiano nao ghafla.

Chanzo - NIPASHE

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post