Chipukizi wa Azam Fc, Yahya Zayd katika moja ya mchezo wa ligi kuu Tanzania bara.
Klabu ya soka ya Azam imemfungulia milango kinda mwingine katika harakati za kucheza soka la kimataifa baada ya dili la Shaban Idd Chilunda kukamilika kwenda nchini Hispania katika klabu ya Tenerife.
Mabingwa hao wapya wa Afrika mashariki na kati wameripotiwa kumruhusu mchezaji chipukizi, Yahya Zayd kwenda nchini Afrika Kusini kwaajili ya majaribio katika klabu ya Bidvest Wists.
Taarifa hiyo imethibitishwa kupitia kwa Afisa habari wa klabu hiyo, Jaffar Idd Maganga ambaye amesema.
“ Yahya Zayd ameondoka kuelekea nchini Afrika Kusini ambako amepata mwaliko wa kwenda kwenye majaribio kwa muda wa wiki moja “. Amesema Maganga.
“ Sisi kama Azam Fc kwetu ni kama fursa na tunamwombea aweze kufaulu majaribio hayo kwani kufaulu kwake ni kufaulu kwa Azam na kama hatofanikiwa basi milango iko wazi kwake kurejea “. Ameongeza .
Maganga pia amezungumzia maandalizi ya klabu hiyo kuelekea msimu mpya wa ligi kuu Tanzania bara ambapo amesema kuwa kwa sasa wako kambini hadi Julai 30 itakaposafiri kwenda nchini Uganda.
Zayd ni mchezaji ambaye amecheza mechi nyingi msimu wa ligi kuu Tanzania Bara uliomalizika na endapo dili hilo litakamilika, atakuwa mchezaji wa pili chipukizi wa Azam Fc kujiunga na klabu ya nje mwaka huu.