Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) taifa Dk. Bashiru Ally amewaapisha wanachama wapya 269 kutoka vyama vya upinzani akiwemo aliyekuwa Mbunge wa jimbo la Kasulu Vijijini Agripina Buyogera na Mwenyekiti wa Chama cha NSSR Mkoa na wilaya ya Kasulu Hitra Joseph Gervas Bahenga katika mkutano wa kampeni za uchaguzi wilayani Kakonko mkoani Kigoma.
Zoezi hilo alilifanya jana katika mkutano wa uzinduzi wa kampeni za ubunge katika uchaguzi mdogo wa jimbo la Buyungu wilayani humo wakati akimnadi mgombea wa chama hicho ambapo wananchi hao waliamua kujiunga naCCM na kuwaomba wananchi kuendelea kukiamini chama hicho na kumpa kura mgombea wa Chama Cha Mapinduzi.
Alisema wanachama hao hawajawanunua bali wamevutiwa na utekelezwaji wa ilani ya chama na amewaahidi wananchi kabla ya uchaguzi huo kuisha watapokea vigogo wengi na watawapokea hawatawabagua wote watakaotaka kujiunga na Chama Cha Mapinduzi na wote wana haki ya kujiunga na chama hicho.
"Milango ya wanachama wapya iko wazi na tunawakaribisha sana na hawa ndiyo wamefungua mlango, tunawakaribisha wote CCM haina mwenyewe wote tuna sifa ya kuwa wanachama sasa tunapokea wote na hatuko tayari kununua watu kutoka vyama vingine wataona mambo wenyewe watakuja", alieleza Dk.Bashiru.
Akimkaribisha mgeni rasmi katika uzinduzi wa kampeni hizo, Kada maarufu wa Chama cha mapinduzi Yusuph Makamba,alisema CCM ni chama cha wanyonge na kipo kwa ajili ya kuwatetea wananchi katika kuleta maendeleo hivyo kuwaomba Wanakakoko kumchagua Chiza ili akafanye kazi na Chama cha Mapinduzi.
Alisema anatambua mchango wa Chiza kwa Wanakakonko na yapo mengi ambayo ameyafanya kwa jimbo la Buyungu, suala la kuwashawishi wananchi wasimchague kwa kigezo kwamba ni mzee hii sio kweli wamuamini wampe kura aweze kuwaletea maendeleo zaidi.
"Tunaye mgombea ambaye tunamnadi kwa sifa zake angalia elimu yake, busara zake, mchango wake katika jamii kupitia mkutano huu wana CCM wote watakaohusika na kampeni muwe na moyo wa kuvumilia mkitupiwa matusi msirudishe matusi hayo CCM ni chama cha wastaarabu muwe wavumilivu" ,alisema Katibu Mkuu.
Alisema serikali imefanya mambo mengi ya maendeleo na anasimamia na utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi chama kinacho fanya kazi ya uongozi katika kusimamia mapambano ya kupunguza umaskini vijijini, ili uweze kuondoa umasikini lazima uwekeze katika elimu ambayo ni sekta mama na serikali imefanya vizuri.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha NCCR Mkoa wa Kigoma James Bahingai alisema ameridhishwa na utendaji wa Rais John Magufuli kwa kazi kubwa anayoifanaya na kutangaza kujiunga na Chama cha Mapinduzi wakati wa uzinduzi huo wa kampeni.
"Rais ameikubali Kigoma kwa kuwapa Mawaziri ni heshima kubwa na nimeahidi kukaa katika jimbo la Buyungu ili kuhakikisha mgombea wa Chama Cha Mapinduzi anapita tunataka kiongozi atakaekwenda kuzungumza na rais mambo yanayofaa", alisema Bahingai.
Naye aliyekuwa mbunge wa jimbo la Kasulu vijijini Agripina Buyogera aliahidi kuendelea kuruka kama ndege na anatua kama ninja kwa dhamira yake ameamua mwenyewe kurudi CCM na kuhakikisha Maendeleo yanapatikana hivyo wampitishe Chiza kwa kuwa ndiye mbunge pekee atakayeweza kuleta maendeleo.
Na Rhoda Ezekiel - Malunde1 blog Kigoma