Mkereketwa wa CCM wa Kata ya Bagara Mjini Babati mkoani Manyara, Hamis Bura akipeperusha Bendera ya Chama hicho wakati wakijiandaa kuelekea katika uzinduzi wa kampeni ya mgombea udiwani wao , Nicodemus Tlaghasi. Picha na Joseph Lyimo-Mwananchi
Wakati CCM ikikusanya kata 19 kwa wagombea wake kupita bila kupingwa katika uchaguzi mdogo wa madiwani, vyama vya upinzani vimeendelea kulia wakidai kuchezewa rafu.
Chama hicho kimepata kata hizo kati ya 77 za uchaguzi huo unaotarajiwa kufanyika Agosti 12,2018.
Huu ni uchaguzi mdogo wa nne wa udiwani kufanyika baada ya Uchaguzi Mkuu wa Rais, wabunge na madiwani wa 2015. Uchaguzi mdogo wa kwanza wa madiwani katika kata 20 ulifanyika Januari 22, 2017 na wa pili wa kata 43 ulifanyika Novemba 26, 2017.
Uchaguzi mdogo wa tatu wa madiwani wa kata nne uliohusisha pia majimbo mawili ya ubunge ya Siha mkoani Kilimanjaro na Kinondoni, Dar es Salaam ulifanyika Februari 17.
Kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ibara ya 76 (3), Sheria ya Taifa ya Uchaguzi (sura ya 343) katika kifungu cha 76 (3) na Sheria ya Uchaguzi ya Serikali ya Mitaa (sura ya 292) katika kifungu 13 (6), chaguzi ndogo za ubunge na udiwani zinafanyika baada ya Uchaguzi Mkuu wa Rais, wabunge na madiwani kupita na hazifanyiki iwapo miezi 12 imebaki kabla Bunge kuvunjwa.
Wakati wagombea wa CCM katika uchaguzi huo wakipita bila kupingwa katika kata hizo, wagombea wengi wa vyama vya upinzani wamejikuta wakikosa sifa za kuteuliwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), baada ya baadhi kushindwa kurejesha fomu, kuwekewa pingamizi na kasoro mbalimbali.
Uchaguzi wa kata hizo na Jimbo la Buyungu utafanyika Agosti 12 huku NEC ikisema imejipanga kikamilifu kuzishughulikia kwa wakati rufaa zote zitakazowasilishwa.
Kati ya kata 19 ambazo CCM imejikusanyia, 11 ni za Jiji la Arusha; tano za Halmashauri ya Mji wa Tunduma mkoani Songwe, mbili ni za Serengeti mkoani Mara na moja ni ya Kimara jijini Dar es Salaam.
Katika Jiji la Arusha ambalo lina kata 20, wagombea wa Chadema waliobaki katika kinyang’anyiro hicho wako tisa.
Msimamizi wa uchaguzi katika Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti, Juma Hamsini alimtangaza mgombea wa Kata ya Ikoma, Michael Kunani na Charles Muyuga wa Manchira kuwa wamepita bila kupingwa.
Alisema mgombea wa Chadema wa Ikoma, Kennedy Josephat hakurejesha fomu huku yule wa Manchira wa chama hicho, Timani Shaweshi akibainika kuidanganya NEC wakati wa ujazaji fomu.
NEC yasubiri rufaa Dar
Akizungumza na Mwananchi juu ya malalamiko yaliyotolewa na wapinzani jana, mkurugenzi wa NEC, Dk Athuman Kihamia alisema wamejipanga kikamilifu kuhakikisha rufaa au malalamiko ambayo yatafika mbele ya tume yanafanyiwa kazi haraka iwezekanavyo.
“Hadi muda huu tunapozungumza (saa 8:42 mchana), bado sijapokea rufaa au pingamizi yoyote na hii inatokana na mapingamizi yanaanza kushughulikiwa ngazi ya kata. Sasa yakipita huko yanakuta tume ambako hayajafika,” alisema.
“Sisi hapa tupo standby (tayari)na zinaweza kufika kesho (leo) kwani ni siku tatu na sisi tunafanyia kazi kile ambacho tunaletewa kwa njia ya maandishi, lakini mitandaoni sijui wapi, si utaratibu.”
Alisema NEC inaendesha uchaguzi kwa kufuata sheria na taratibu na kama hakuna kilichofika kwa maandishi ofisini inakuwa vigumu kujibu au kukizungumzia.
“Tunasubiri rufaa na tutazijibu kwa wakati zikifika na ninachoweza kusema tume itajitahidi kwa asilimia 100 kutumia sheria na taratibu ili haki iweze kutendeka kwa kila mmoja na uchaguzi ufanyike kama ulivyopangwa,” alisisitiza Dk Kihamia.
Kilio cha wapinzani
Chama cha ACT-Wazalendo, kilisema jana kuwa hujuma, rafu na hila zinaendelea katika uchaguzi huo na ni sababu iliyowafanya wao na Chadema kusimamisha wagombea kwa hatua za awali.
Sababu nyingine ni namna ya NEC ilivyotoa muda wa wiki moja kuchukua fomu na kuzirejesha, jambo lililosababisha vyama hivyo kukosa muda wa kukaa na kukubaliana jinsi ya kusimamisha wagombea katika uchaguzi huo.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, mwenyekiti wa Kamati ya Kampeni ya Uchaguzi wa ACT-Wazalendo, Mohamed Babu alisema ingawa viongozi wapo katika mazungumzo ya hatua za mwisho, lakini wamefikia uamuzi wa kushirikiana ili kukabiliana na hujuma mbalimbali zinaoendelea.
“Mazungumzo ya ushirikiano sasa hivi yapo katika hatua ya pili ambayo ni kufanya tathmini ya kila mgombea aliyependekezwa na chama husika na kuungwa mkono. Hatua ya mwisho ya mazungumzo haya ni vyama hivi kukubaliana kusimamisha mgombea mmoja,” alisema.
Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mawasiliano kwa Umma wa chama hicho, Ado Shaibu alisema ACT-Wazalendo inasikitishwa na rafu na hujuma zinazoendelea kufanywa dhidi ya wapinzani.
Kwa upande wao, Chadema wamekata rufaa kupinga kuenguliwa kwa mgombea udiwani wa chama hicho Kata ya Kelamfua Mokala wilayani Rombo.
Katibu wa chama hicho Mkoa wa Kilimanjaro, Basil Lema alisema kutoteuliwa kwa mgombea wao, Emmanuel Tarimo ni nia ovu ya msimamizi wa uchaguzi katika Halmashauri ya Wilaya ya Rombo, Magreth John.
Lema alisema msimamizi huyo ambaye ni mkurugenzi wa halmashauri hiyo, alipora madaraka ya msimamizi msaidizi wa uchaguzi ambaye ni mtendaji wa kata na kutangaza kutomteua mgombea wa Chadema, jambo ambalo ni kinyume cha utaratibu.
“Tuna mashaka na msimamizi wa uchaguzi na tumebaki tunajiuliza maswali mengi, kwa nini alitoa barua ya kutoteuliwa wakati jina la mgombea wetu halijawekwa kwenye ubao wa matangazo,” alisema Lema.
Alisema tayari amemuagiza katibu wa Chadema Wilaya ya Rombo kuandika barua ya kumkataa msimamizi wa uchaguzi katika kata hiyo kwa kuwa hawana imani naye.
Kumekucha Kyela
Wakati maeneo mengine kukiwa na mvutano, CCM na Chadema Kata ya Kyela mjini mkoani Mbeya vimetangaza siku za kuzindua kampeni baada ya kupitishwa kwa wagombea wao.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, viongozi wa vyama hivyo walisema michakato yote imekamilika na sasa wameanza kampeni za chinichini.
Katibu wa Chadema Wilaya ya Kyela, Donald Mwaisango alisema baada ya kukamilisha masuala yote ya uteuzi wa mgombea ndani ya chama na NEC kumpitisha Kanyiki Andembwise, jana walitarajia kuzindua kampeni zao.
Naye katibu wa CCM Wilaya ya Kyela, Christina Kibiki alisema wanatarajia kuzindua kampeni Jumamosi wiki hii, lakini kwa sasa wanafanya kazi ndogondogo huku wakiendelea kuwahamasisha watu kushiriki vyema kuanzia kampeni hadi siku ya kupiga kura.
Alisema mgombea wao, Alex Mwinuka alipitishwa na vikao halali vya CCM na wana imani kampeni zao zitakuwa na utulivu pamoja na amani.
Wakati hayo yakiendelea wilayani humo, Chadema wilayani Babati mkoani Manyara imewataka viongozi wa Serikali ngazi ya wilaya na mkoa kuwaachia wanasiasa pekee kampeni za uchaguzi huo na kutouingilia.
Katibu wa Chadema wa mkoa huo, Gervas Sulle alisema endapo viongozi wa Serikali wasipoingilia wana uhakika wa kutetea kata zao na kushinda.
Msigwa atoa neno
Mbunge wa Iringa Mjini (Chadema), Mchungaji Peter Msigwa akizungumza na waandishi wa habari mjini humo jana, alielezea jinsi wagombea wao wanavyokatwa huku akisema CCM haiwezi kuingia kwenye uchaguzi na ikashinda uchaguzi ukiwa wa haki.
Alisema zimefanyika njama ovu za kuwakata wagombea wao katika kata za Gangilonga na Kwakilosa.
“Pamoja na kuporwa haki zetu katika kata mbili ya Gangilonga na Kwakilosa tunaahidi Chadema kuingia kwa nguvu zetu zote katika uchaguzi wa kata zingine tatu za mjni Iringa ambazo ni Ruaha, Mkwawa na Mwangata na tutashinda kwa haki,” alisema
“Mkurugenzi tunaomba atende hali na afuate sheria za uchaguzi, asifanye kazi kwa shinikizo la CCM na Jeshi la Polisi lisimamie misingi yake ya kulinda wananchi wote na si kufanya kazi ya chama tawala. Hata wapinzani ni wananchi kama walivyo CCM,” alisema Msigwa.
Akijibu tuhuma hizo, msimamizi wa uchaguzi Jimbo la Iringa mjini, Omari Mkangama ambaye pia ni kaimu mkurugenzi wa Manispaa ya Iringa alisema kulikuwepo na upotevu wa fomu za wagombea wa Chadema katika kata za Kwakilosa na Gangilonga.
“Baada ya kuwa na upotevu huo ikabidi niwaelekeze Chadema kufuata taratibu ikiwemo kuripoti polisi ndipo walijikuta wapo nje ya muda wa urejeshaji fomu,” alisema Mkangama
“Sijapendelea wala sijashirikisha dola katika kudhulumu haki, naamini nimetenda haki mpaka tunatangaza wagombea wa CCM wamepita bila kupigwa ni kwa kuwa hakuna mgombea wa Chadema aliyerudisha fomu.”
Imeandikwa na Ibrahim Yamola na Bakari Kiango (Dar), Maryasumta Eusebi (Moshi), Berdina Majinge (Iringa), Joseph Lyimo (Babati), Godfrey Kahango (Mbeya) na Anthony Mayunga (Serengeti)