DKT. NDUMBARO ATOA USHAURI ELIMU YA KODI SHULENI


Mbunge wa Songea Mjini Mhe. Dk. Damas Ndumbaro akisisitiza jambo wakati akizindua mashindano ya vilabu vya Kodi kwa Shule za Sekondari katika Tamasha la Majimaji Serebuka linaloendelea Songea Mkoani Ruvuma. (Picha zote na Oliver Njunwa) 
Baadhi ya wanafunzi wa shule za sekondari mkoani Ruvuma wakifuatilia mashindano ya Vilabu vya Kodi kwa shule za Sekondari katika ukumbi wa Chuo cha Ualimu Songea. 
Mratibu wa Mashindano ya Vilabu vya Kodi kwa Shule za Sekondari Mkoani Ruvuma Njovu Kilian akifafanua jambo kwa wananfunzi. Wengine ni Mbunge wa Songea Mjini Mhe. Dk. Damas Ndumbaro (katikati) na Mwakilishi wa Benki ya NMB. 
Wawakilishi wa Shule za Sekondari ikiwasilisha mada wakati wa Mashindano ya Vilabu vya Kodi kwa shule za Sekondari. 
Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi Richard Kayombo akizungumza na wanafunzi (hawapo ktk picha) walioshiriki mashindano ya Vilabu vya Kodi kwa Shule za Sekondari katika Tamasha la Majimaji Serebuka Mkoani Ruvuma. Waliokaa kutoka (kushoto) ni Meneja wa TRA Mkoa wa Ruvuma, Rosalina Mwenda na Mratibu wa Mashindano ya Vilabu vya Kodi katika Shule za Sekondari TRA Njovu Kilian. 
 *****
Wanafunzi katika shule za sekondari wanatakiwa kufahamu masuala na umuhimu wa kodi kutokana na juhudi ambazo Serikali ya Awamu ya Tano imefanya katika kutoa elimu ya msingi na sekondari nchini bure

Ushauri huo umetolewa na Mbunge wa Songea Mjini Mhe. Dk. Damas Ndumbaro wakati akizindua rasmi mashindano ya vilabu vya kodi kwa shule za sekondari katika Tamasha la Majimaji Serebuka linaloendelea Songea katika Mkoa Ruvuma.

Mhe. Ndumbaro amesema kwamba kutokana na kukosa mtaala wa elimu ya kodi katika shule za sekondari, Mkoa wa Ruvuma uliamua kuwa na mdahalo wa masuala ya kodi kwa shule za sekondari ili wanafunzi waweze kufundishana kwani katika kuwasilisha mada za masuala ya kodi wanafunzi wanajifunza na kufundishana.

“Samaki mkunje angali mbichi. Umri wa vijana walio sekondari ni umri mzuri wa kuwaelimisha masuala ya kodi”, alisema Dk. Ndumbaro na kuongeza kwamba wanafunzi wakifundishana wenyewe kwa wenyewe wataelewa zaidi kuliko wanapofundishwa.

Mbunge huyo wa Songea Mjini alisema kwamba wanafunzi wanatakiwa kufahamu kwamba gharama ya elimu ya bure inayotolewa katika shule za msingi na sekondari, ujenzi wa viwanja vya ndege, barabara, ununuzi wa ndege, na upatikanaji wa umeme katika Mkoa wa Ruvuma wa gridi ya taifa kutoka Makambako zinatokana na kodi.

Aidha amewataka wanafunzi kushiriki vizuri katika mdahalo huo bila kujali kwamba watashinda au la kwani kwa kuweza kufikia hatua ya ushiriki tayari wote ni washindi Mdahalo huo unaohusu mashine za risiti za kielektroniki na umeandaliwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa kushirikiana na waandaji wa Tamasha la Serebuka.

Naye Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania Richard Kayombo amewataka wanafunzi kuelimisha jamii inayowazunguka kuhusu masuala ya kodi kwani kodi ndio pato pekee linaloiwezesha nchi kuhudumia wananchi wake.

“Sisi tutaendelea kutoa elimu kwa kadiri ya uwezo wetu bila kuchagua na nyinyi tunawaandaa ili muweze kutoa elimu kwa familia zenu, majirani zenu, wanafunzi wenzenu na jamii nzima inayowazunguka”, alisema Kayombo.

Amewataka wanafunzi kudai risiti wanaponunua bidhaa, kulipa kodi wakati wa kulipa kodi ukifika kwani wanafunzi ni wafanya biashara na walipakodi watarajiwa.

Naye Mratibu wa Mashindano ya Vilabu vya kodi katika Tamasha hilo kutoka TRA Njovu Kilian amesema kwamba Mashindano hayo yamekuwa na mwamko mzuri kutokana na kuongezeka kwa washiriki. “Mwaka jana tulikuwa na washiriki 22 lakini mwaka huu tuna shule 32 ambazo zinashiriki”, alisema Njovu.

Pamoja na kushindana kuwasilisha mada pia kutakuwa na shindano la kuchora katuni inayohusu masuala ya kodi

Mashindano ya Vilabu vya Kodi katika shule za Sekondari katika Tamasha la Serebuka yanashirikisha shule za Sekondari 32 za Mkoa wa Ruvuma ambapo baada ya mchujo shule sita bora zitaingia fainali na kushindana kupata shule tatu bora.

Katika mashindano haya washindi watapata zawadi ya pesa taslimu kuanzia shilingi laki mbili hadi elfu hamsini ambazo zinatolewa na TRA na Benki ya NMB kwa uande wao watatoa zawadi ya kuwafungulia akauti washindi wa jumla watano pamoja na zawadi nyingine.

Washindi wapo katika makundi sita ambayo ni wawasilishaji bora wa mada, washindi wa jumla, walimu bora, shule bora, mwanafunzi aliye wasilisha mada vizuri, na mchoraji mzuri wa katuni.

Mashindano haya ambayo yanaandaliwa na TRA kwa kushirikiana na Songea Mississippi (SOMI) ambao ni waandaaji wa Tamasha la Serebuka yanafanyika kwa mara ya pili tangu yaanzishwe Mwaka 2017 mkoani Ruvuma ambapo shule za sekondari hufanya mdahalo kuhusu mada yoyote ya kodi iliyochagauliwa na washindi hupata zawadi. Mada inayojadiliwa katika mashindano ya mwaka huu ni ‘Mashine za Kodi za Kielektroniki’

(Imeandaliwa na Robert Okanda)

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post