Teknolojia ya kutambua nyuso za watu inaendelea kuimarika kila siku, huku baadhi ya kampuni zikisema kuwa sasa zinaweza kusoma hisia na kutambua tabia zinazotiliwa shaka.
Hata hivyo, teknolojia hiyo ya kutambua sura imekuwepo kwa miongo kadhaa, lakini imekuwa ikiimarika polepole katika miaka ya hivi karibuni kutokana na maendeleo katika maono ya kompyuta na mfumo wa mitambo inayoweza kufikiria kama binadamu.
Wataalamu katika eneo hilo wanasema teknolojia hiyo sasa inatumika kuwatambua watu mipakani, kufungua simu aina ya Smartphone, kuwakamata wahalifu na kuelezea waliohusika katika mambo mbalimbali ya kibenki.
Maendeleo ya teknolojia yamezifanya baadhi ya kampuni kubainisha kuwa zinaweza hata kutambua hisia za watu.
Tangu 1970, wanasaikolojia wanasema wamefanikiwa kugundua hisia zilizojificha kwa kusoma hisia katika uso wa mtu, ndani ya picha ama video.
Kwamba kamera za kiwango cha juu, zinaweza kubaini hilo vizuri na kwa haraka.
Na duka la jumla, linaweza kuzitumia kamera hizo katika njia zilizopo katikati ya bidhaa zake, sio kutambua watu, lakini kubaini aliyeingia ndani kutokana na umri na jinsia pamoja na hisia zake.
Aidha, zinaweza kutumika katika ukuzaji wa bidhaa na uwekaji wa bidhaa mpya.
Kampuni ya utafiti wa soko ya Kantar Millward Brown, inatumia teknolojia iliyovumbuliwa na kampuni moja ya Marekani, kubaini vile wateja wanavyoitikia matangazo ya runinga.
Kampuni hiyo inarekodi kanda za video za nyuso za watu kwa ruhusa yao, na baadaye kuchunguza hisia zao kwa kutumia fremu za siri, ili kubaini hisia zao.
“Sisi huwahoji watu, lakini tunawaelewa zaidi kwa kuangalia hisia zao. Unaweza kuona ni eneo gani la tangazo linalofanya vyema na hisia zinazotolewa,” anasema Graham Page, Mkurugenzi Mkuu katika kampuni hiyo ya Kantar Millward Brown.
USALAMA
Mbali na hilo, teknolojia hii inaweza kutumika kutambua hisia kwa lengo la kuimarisha usalama, kwa mujibu wa baadhi ya kampuni zinazoendeleza teknolojia hii.
Kwa mfano kampuni ya Uingereza ya WeSee, inasema kuwa teknolojia yake inayofikiria kama binadamu, inaweza kugundua tabia zinazotiliwa shaka kwa kusoma hisia zisizoweza kuonekana na jicho la kawaida.
Hisia kama vile wasiwasi na hasira, zinaweza kufichwa, ikilinganishwa na lugha inayozungumzwa.
WeSee inasema kuwa imekuwa ikishirikiana na shirika kubwa la kuhimiza sheria kufuatwa, kuwachunguza watu wanaofanyiwa mahojiano.
Katika siku zijazo kamera za kanda za video katika kituo cha reli, zinaweza kutumika kutambua tabia inayotiliwa shaka na kuripoti kwa mamlaka kuhusu tishio la kigaidi.
Hata hivyo, wataalamu wanasema pamoja na utafiti kutoa fursa ya kutumika kwenye makundi ya watu katika hafla kama vile kandanda ama mikutano ya kisiasa, kuna shaka juu ya uhakiki wa hisia zinazogunduliwa.
Wanasema wakati unapotaka kutambua nyuso pekee, kuna makosa machache hutokea na hilo linathibitishwa na kampuni bora zaidi katika eneo hilo zinazodai kwamba zinaweza kutambua watu kwa asilimia 90 hadi 92.
“Unapojaribu kuchunguza hisia, makosa makubwa hupatikana,” zinabainisha.
ZILIKOTUMIKA
Wakati watazamaji walipohudhuria hafla ya BBC Radio 1's mjini Swansea nchini Uingereza, mwezi Mei, wengi hawakujua kwamba sura zao zilikuwa zikichunguzwa, ukiwa ni miongoni mwa uchunguzi mkubwa uliofanywa na maofisa wa polisi wa South Wales.
“Mtu mmoja ambaye alikuwa akitafutwa aligunduliwa na kukamatwa ndani ya kipindi cha dakika 10, baada ya teknolojia hiyo kuwekwa katika tamasha hilo la muziki,” anasema Scott Lloyd, kiongozi wa mradi wa maofisa wa polisi wa South wales.
Hata hivyo, kundi la haki za binadamu la Liberty, linasema kuwa teknolojia hiyo imepokea majibu yasiyo sahihi katika michuano kama ile ya klabu bingwa Ulaya, katika uwanja wa Cardif, mwaka jana.
Na mnamo mwezi Julai, wakazi wa Cardiff Ed Bridges, wanaowakilishwa na Liberty, walianza kuchukua hatua za kisheria dhidi ya kikosi hicho, wakidai kwamba kitendo cha maofisa hao kinakiuka faragha, hatua iliyosababisha kesi kuwasilishwa mahakamani. BBC