Na Felix Mwagara, MOHA
WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola ameipa wiki mbili Kampuni ya Kimataifa ya Iris Corporation Berhard impe majibu ya kuwa italeta mtambo wa kutengeneza kadi ghafi au Dola za Marekani Milioni 14 sawa na zaidi ya shilingi bilioni 32 za Tanzania.
Akizungumza na waandishi wa habari katika ukumbi wa mikutano wa Wizara hiyo, jijini Dodoma jana, mara baada ya kumaliza kikao na Menejimenti ya Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) pamoja na viongozi wa Kampuni hiyo, Waziri Lugola alisema kampuni hiyo haiwezi ikacheza na fedha za Watanzania ambao ni za walipa kodi.
Lugola aliongeza kua lazima fedha hizo au mtambo huo upatikane kwa kuwa Serikali ya Awamu ya Tano haitakubaliana na mchezo mchafu wa aina yoyote, na pia yeye kama Waziri wa Wizara hiyo anaendelea kutekeleza maagizo ya Rais Dkt John Magufuli.
“Tumezungumza nao na tumekubaliana nao kwamba tuwape wiki mbili ili bodi ya kampuni hiyo ikakae ifanye maamuzi ya aidha waturudishie fedha zetu au walete mtambo, lakini sisi kama nchi huu mtambo muhimu sana, bado tuna uhitaji, sisi tungependa baada ya hiyo wiki mbili wafanye maamuzi ya kutuletea mtambo,”alisema Lugola.
Aidha, Waziri Lugola amewataka wamiliki wa kampuni zilizolipwa kifisadi fedha za Mradi wa mtambo wa NIDA kujisalimisha jijini Dodoma Agosti 3 mwaka huu wakiwa na mtambo huo vinginevyo warejeshe fedha zilizotumika.
Pia Lugola ametoa agizo kwa aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa NIDA, Dickson Maimu na Mfanyabiashara Jack Gotham kufika ofisini kwake Agosti 3 saa 3:00 asubuhi ili kutoa maelezo yanayojitosheleza yatakayomsaidia kutoa maamuzi sahihi kuhusiana na ufisadi wa fedha zaidi ya bilioni 32 za mtambo huo ambao hadi sasa haujafika nchini.
Lugola aliyataja kampuni hayo kuwa Gotham International ambayo imelipwa kifisadi shilingi 2,848,878,659.75, Iris Corporation Berhard ambayo imelipwa kifisadi 22,919,414,169,84, Gwiholoto Impex inayodaiwa shilingi 946,406,989,00, Sykes Travel Agent 5,979,600,00, Dk Shija Paul Rimoy 27,000,000,00, Aste Insurance 1,206,619.93, na Kampuni ya BMTL 569,192,090,00.
Hata hivyo, Waziri Lugola aliwataka Watanzania kutowahusisha viongozi wa sasa wa NIDA na ufisadi huo kwa kuwa hawahusiki hata kidogo, matukio yote ya ufisadi yamefanywa na watangulizi wao na viongozi waliopo sasa wameletwa kuiongoza Mamlaka hiyo kwa ajili ya kuboresha utendaji wa NIDA.