KIGWANGALLAH: MIFUGO ITAKAYOKAMATWA KWENYE MAENEO YA HIFADHI ITATAIFISHWA BILA YA HURUMA

Na Hamza Temba, Nkasi Rukwa
...............................................
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla ametangaza zoezi rasmi la kuanza kutaifishwa mifugo itakayokutwa kwenye maeneo ya hifadhi nchini kinyume cha sheria ili kukomesha vitendo hivyo.


Dk. Kigwangalla ametoa tamko hilo jana alipokuwa akizungumza na wananchi wa kijiji cha Kizi kinachopakana na Pori la Akiba Lwafi lililopo wilaya ya Nkasi mkoani Rukwa, wakati wa ziara yake ya kikazi ya siku moja wilayani humo .


Amesema Sheria ya Wanyamapori Namba 5 ya mwaka 2009, Kifungu cha 111 kinaruhusu kutaifisha mifugo na mali itakayokamatwa hifadhini.


Amesema kwa kipindi cha miezi tisa tangu ateuliwe kuiongoza wizara hiyo amekuwa akitoa msamaha kwa wnanchi wanaakamatwa na mifugo hifadhini jambo ambalo kwa sasa hatofanya tena kwakuwa elimu imeshatolewa vya kutosha.


"Maeneo ya hifadhi sio shamba la bibi lisilokuwa na mwenyewe, ni lazima watu waheshimu sheria za uhifadhi, nawahakikishia tukiwakuta kwenye maeneo ya hifadhi, tutawakamata na kutaifisha mifugo yenu, hakutakuwa na huruma wala msalia mtume" alisisitiza Dk. Kigwangalla.


Wakati huo huo Dk. Kigwangalla ameiagiza Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) kuwasilisha ahadi iliyotolewa na Waziri aliyemtangulia ya shilingi milioni 3 kwa ajili ya kusaidia ujenzi wa mradi wa maji katika kijiji cha Kizi. Pia ameiagiza mamlaka hiyo kuchangia mabati kwa ajili ya darasa moja katika kijiji hicho ili wananchi wanufaike na faida inayopatikana kwenye uhifadhi.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post