Waziri wa Kilimo Dk Charles Tizeba amewataka watafiti wa Kilimo kupeleka matokeo ya utafiti wanaoufanya kwa wakulima wanaowazunguka.
Ametoa kauli hiyo jana Ijumaa Julai 20, 2018 katika maonyesho ya Kilimo cha biashara jijini Arusha.
Amesema kwa muda mrefu watafiti wa kilimo wanajifungia na tafiti zao huku jamii iliyowazunguka ikzalisha mazao machache.
"Bahati mbaya hakuna uhusiano kati ya watafiti na wakulima. Watafiti wanafanya kivyao na wakulima kivyao," alisema Dk Tizeba.
“Kuna kituo cha utafiti cha Seliani lakini ukienda King'ori tu hapo, hoi. Utakuta kuna mkulima yuko nje ya wigo wa taasisi miaka 30, anacholima ni tofauti kabisa. Kuna kituo cha utafiti wa kahawa (Tacri) lakini wakulima wa kahawa wanalia.”
Amewataka watafiti kubadilisha mtazamo na kuacha kujifungia na tafiti zao.
"Kuna mahindi lishe hapa, yapo miaka tisa nani anajua? Msipobadilisha mtazamo tutabaki na maprofesa wenye vyeti tu," alisema.
Amevitaka vituo vya utafiti kufanya biashara ya mazao wanayozalisha badala ya kusubiri kupata fedha za Serikali kujiendesha.