Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

KINONDONI NA FUMBO NA UTEUZI WA WAKUU WA MIKOA

Na Peter Elias, Mwananchi 
Kwa kutazama mwenendo wa uteuzi, unaweza kusema Wilaya ya Kinondoni ni chuo cha kupika viongozi na hasa wakuu wa mikoa.


Kinondoni ina changamoto na sifa nyingine ambazo pengine ndicho kipimo cha uongozi kwa wanaoteuliwa na Rais kuongoza wilaya hiyo na baadaye kupandishwa hadhi ya kuongoza mikoa.


Kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012, Kinondoni ilikuwa wilaya yenye watu wengi zaidi nchini wakiwa 1,775,049 ikifuatiwa na Temeke (watu 1,368,881) na Ilala (watu 1,220,611).


Hata hivyo, sasa Mkoa wa Dar es Salaam una wilaya tano baada ya Kinondoni kugawanywa na kuunda mpya ya Ubungo na Temeke kumegwa na kuunda Wilaya ya Kigamboni.


Kinondoni pia inakabiliwa na changamoto kadhaa zikiwamo miundombinu mibovu inayosababisha wananchi kuathiriwa na mafuriko ya mara kwa mara na inakabiliwa pia na migogoro mingi ya ardhi.


Kumbukumbu zinaonyesha kuwa mwaka 2011 Rais wa wakati huo, Jakaya Kikwete alimteua Jordan Rugimbana kuwa Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, akipokea kijiti kutoka kwa Kanali Fabian Massawe ambaye aliteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Kagera.


Februari 23, 2015, Kikwete alimteua Paul Makonda kuwa Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni. Katika mabadiliko hayo, Rugimbana aliachwa lakini Septemba mwaka huohuo akateuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Lindi.


Machi 13, 2016 Makonda aliteuliwa na Rais John Magufuli kuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam na nafasi yake kuchukuliwa na Ally Hapi na katika uteuzi uliofanywa juzi na Rais Magufuli, Hapi ameteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Iringa akichukua nafasi ya Amina Masenza ambaye amestaafu.


Hapi ameiongoza wilaya hiyo kwa miaka miwili na nusu na amepokewa kijiti na Daniel Chongolo akitokea Wilaya ya Longido.


Baadhi ya wadau na wasomi waliozungumza na Mwananchi jana kuhusu mwenendo huo wa uteuzi walisema Wilaya ya Kinondoni ina sifa na changamoto zinazomjengea uwezo kiongozi.


Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Udsm), Dk Benson Bana alisema Kinondoni ndiko wanakoishi viongozi wengi wa Serikali, hivyo inahitaji uangalizi wa pekee.


Alisema wilaya hiyo imekuwa ikikabiliwa na changamoto kadhaa kama vile matukio ya ujambazi na migogoro ya ardhi na pia inakabiliwa na utendaji duni wa Serikali za Mitaa.


“Wilaya ya Kinondoni ndiyo kubwa kwa Dar es Salaam ikiwa na idadi kubwa ya watu. Hilo linasababisha iwe na changamoto nyingi za ujambazi na migogoro mingi ya ardhi. Inataka mtu ambaye anatambua changamoto zote hizo,” alisema Dk Bana.


Alisema mkuu mpya wa wilaya hiyo, Chongolo ana kazi ya ziada ya kufanya na hasa wakati huu ambao vyama vya upinzani vinataka kuendesha shughuli zake kama vile kufanya mikutano.


Dk Bana alisema mkuu mpya wa wilaya anatakiwa kusimamia ulinzi na usalama ili kuondoa matukio ya uhalifu ambayo mara nyingi yamekuwa yakiripotiwa. Sambamba na hilo alimtaka kuongeza kasi kwenye utatuzi wa migogoro ya ardhi.


“Akitekeleza hayo ataweza kuwa kama waliomtangulia. Changamoto za Kinondoni ni nyingi na zinahitaji mtu makini, mwenye mikakati ya kiutendaji,” alisema Dk Bana.


Profesa Gaudence Mpangala kutoka Chuo Kikuu cha Katoliki cha Ruaha (Rucu) alisema mkuu wa wilaya anapandishwa cheo kutokana na utendaji mzuri katika maeneo mbalimbali.


Alisema kwa kuangalia siasa za sasa, Wilaya ya Kinondoni na Mkoa wa Dar es Salaam kwa jumla unaongozwa na upinzani, hivyo huenda Hapi alifanya kazi nzuri ya kuudhibiti upinzani na kupelekwa sehemu nyingine ambayo nayo upinzani unaongoza halmashauri.


“Kingine ninachokiona ni utendaji wao mzuri, jiji kubwa kama la Dar es Salaam lina changamoto nyingi, kwa hiyo ukifanikiwa kuzikabili ipasavyo na Rais akaona unachokifanya, atakupandisha cheo,” alisema Profesa Mpangala.


Akizungumzia mwenendo wa uteuzi wa watangulizi wake, Chongolo alisema si lazima iwe hivyo kwa sababu Rais anateua mtu anayeamini atamsaidia kazi.


Alisema kinachozingatiwa ni mazingira ya eneo na uwezo wa mhusika.


“Si lazima iwe hivyo, mbona wilaya niliyotoka (Longido) watangulizi wangu wote walistaafu baada ya kutoka pale lakini mimi nimehamishwa? Rais anateua kwa kuangalia mazingira na competence (uwezo) ya mtu. Ninamshukuru kwa kuniteua, sitamwangusha,” alisema.


Chongolo alisema amepata bahati ya kuishi Mkoa wa Dar es Salaam kwa muda mrefu, hivyo anaifahamu vizuri Wilaya ya Kinondoni na changamoto zake hasa katika elimu, afya na miundombinu.


Alisema atahakikisha anasimamia miradi yote iliyopo katika wilaya hiyo ili ilete tija kwa watu kama ilivyokusudiwa.


Chongolo ambaye pia ni mwanahabari aliahidi kuendeleza juhudi zilizofanywa na mtangulizi wake katika kusimamia utendaji wa Serikali.


“Kuna mradi wa Soko la Magomeni ambao umetengewa Sh9 bilioni, nitakwenda kuusimamia kikamilifu. Wale wanaofikiria kufanya mambo ya kijanja janja hawatakuwa na nafasi,” alisema.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com