Mfanyabiashara Peter Zakaria anayeshikiliwa na polisi kwa mahojiano akituhumiwa kuwajeruhi kwa risasi watu wanaodaiwa kuwa maofisa wa usalama wa Taifa amehamishiwa mjini Musoma.
Awali, Zakaria anayemiliki kampuni ya mabasi ya Zakaria alikuwa akishikiliwa katika kituo cha polisi mjini Tarime anakodaiwa kukabidhiwa na watu wanaodaiwa kuwa maofisa wa usalama wa Taifa, ikielezwa kuwa walimdhibiti baada ya kuwajeruhi wenzao.
Akizungumza Jumamosi Juni 30, 2018 Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Tarime/Rorya, Henry Mwaibambe amethibitisha mfanyabiashara huyo kuhamishiwa mjini Musoma, lakini hakueleza sababu za kuhamishwa kwake.
Tukio la kushikiliwa kwa Zakaria limeibua sintofahamu kutokana na taarifa za awali kudai mfanyabiashara huyo alitekwa na watu wasiojulikana alipokuwa ofisini kwake katika moja ya vituo vyake vya mafuta mjini Tarime.
Taarifa za kudaiwa kutekwa zimeibua taharuki miongoni mwa wananchi na hasa wafuasi na wanachama wa CCM ambao waliingia mitaani na wengine kujaa eneo la hospitali ya wilaya ya Tarime baada ya kuwapo fununu kuwa amelazwa kutokana na majeraha aliyopata baada ya kukamatwa na watu wasiojulikana.
Hata hivyo, jana mchana akizungumza na waandishi wa habari Mkuu wa Mkoa wa Mara, Adam Malima amesema mfanyabiashara huyo amekamatwa na maofisa wa usalama na kufikishwa kituo cha polisi mjini Tarime kwa ajili ya kuhojiwa akituhumiwa kuwajeruhi kwa risasi maofisa wawili wa idara hiyo.
Amesema kabla ya tukio hilo, maofisa watano wa usalama walifika katika kituo cha mafuta kinachomilikiwa na Zakaria kwa nia kujaza mafuta kwenye gari lao
“Wenzao wawili walishuka kwenye gari ghafla wakashambuliwa kwa risasi na Zakaria aliyekuwepo eneo hilo,” amesema Malima.
"Baada ya wenzao kujeruhiwa kwa risasi, maofisa wengine walifanikiwa kumdhibiti Zakaria na kumtia mbaroni na kumkabidhi kwa polisi wanaoendelea kumhoji.”
Malima hakutaka kulizungumzia kwa undani tukio hilo lililotokea juzi Juni 29, 2019 saa 2:30 usiku na kubainisha kuwa waliojeruhiwa wamelazwa katika hospitali ya Wilaya ya Tarime huku mmoja akidaiwa kuwa katika hali mbaya.
Social Plugin