Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola amemuagiza Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania (IGP) Simon Sirro kumpeleka ofisini kwake mmiliki wa kampuni ya Lugumi, Said Lugumi.
Amesema Lugumi anatakiwa kufika katika ofisi yake iliyopo mjini Dodoma Julai 31, 2018 saa 2 asubuhi.
“Waliopita hawakuwa maninja sasa ameingia ninja namtaka Lugumi aje muda ukifika tutawaambia Watanzania,” amesema.
Waziri Lugola ametoa kauli hiyo leo mbele ya waandishi wa habari alipokuwa akitoa tathmini ya ziara aliyoifanya kuanzia Julai 11, 2018 kwenye taasisi mbalimbali zilizo chini ya wizara yake.
Pia amemuagiza Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida), Andrew Massawe kufika ofisini kwake Julai 25, 2018 mjini Dodoma akiwa na mtambo wa kutengeneza vitambulisho vyaTaifa au kampuni ikiwa na fedha hizo.
Amesema kuna kampuni iliyopewa jukumu la kuleta mtambo kwa ajili ya vitambulisho hivyo na muda umeisha bila mtambo huo kuonekana.
“Afike ofisini kwangu mjini Dodoma pamoja na watu waliopewa tenda hiyo waje na mtambo au fedha hizo kiasi cha Sh32 bilioni,”amesema Lugola.
Amesema watu hao kama hawana fedha au mtambo basi wawe na maelezo yatakayojitosheleza kwa nini mtambo huo haujawasili hadi leo.