KANGI LUGOLA : SIPO TAYARI KUTUMBULIWA...NITAWATOA MATUMBO WENYE KAULI ZA UCHOCHEZI


Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola amevionya vyama vya siasa kwa kusema hayuko tayari kutumbuliwa ila atawatoa ‘matumbo’ watakaotoa kauli za uchochezi kwenye kampeni.

“Siko tayari kutumbuliwa ila niko tayari kuwatoa matumbo wote watakaokuwa wanajihusisha na uchochezi kabla tumbo langu halijatumbuliwa na mheshimiwa Rais,” alisema Lugola alipozungumza na waandishi wa habari jana mjini hapa.

Kauli hiyo ya kuvionya vyama vya siasa imekuja wakati vyama hivyo vipo kwenye kampeni ya uchaguzi mdogo wa madiwani na ubunge, utakaofanyika Agosti 12.

“Navionya vyama vyote vya siasa, mtu yoyote wa chama chochote cha siasa atakayeonekana akitumia kinywa chake kutoa matamko ambayo ni ya uchochezi ajue kwamba hayuko salama tutavikamata hata kama ni mgombea yuko katika jukwaa,” alisema.

Lugola alisema mgombea atakayetoa matamshi ya uchochezi atakamatwa na huenda akakosa haki ya kuendelea na uchaguzi.

“Hii ni kwa sababu haturuhusu mtu atoe matamshi ya kutukana viongozi, matamshi ya uchochezi atakuwa amepoteza nafasi yake ya kuomba kura labda bahati yake kama wananchi wanamtaka kumchagua bila kuendelea na kampeni,” alisema.

Alionya kuwa asisikie mtu yoyote anatoa kauli ya uchochezi atapambana naye na kwamba yeye aliapishwa na Rais John Magufuli ili kuhakikisha kuwa nchi inakuwa na amani, usalama na utulivu.

Lugola alisema pia Rais Magufuli wakati anaapishwa kushika uongozi wa nchi, aliahidi kuendelea kudumisha uhuru, amani, usalama na kuwalinda Watanzania.

Alisema hayuko tayari kuwafumbia macho wanaofanya uchochezi kwa kuwa huko itakuwa ni kumuangusha Rais Magufuli.

Na Sharon Sauwa, Mwananchi

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post