Mchimbaji wa madini ya rubi, Baraka Lenguti (28) mkazi wa Wilaya ya Siha amefariki wakati akiwa ndani ya mgodi wilayani Longido, huku mwenzake akiachwa mahututi baada ya kuvuta hewa ya sumu mgodini.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Ramadhani Ng’azi, amethibitisha kutokea kwa kifo hicho, kilichotokea majira ya saa 6 – 7 usiku wa kuamkia Julai mosi.
Mgodi huo uliopo kijiji cha Mundarara, wilayani Longido unamilikiwa na mfanyabiashara, Gabriel Sendeu wa jijini Arusha.
Kamanda Ng’azi alisema mwili wa marehemu ulichukuliwa na askari polisi wa Longido kwa ajili ya uchunguzi na baada ya kukamilika taratibu utakabidhiwa kwa ndugu zake kwa ajili ya maziko.
Kuhusu mchimbaji ambaye hali yake ni mbaya, amelazwa katika hospitali ya Longido na kwamba jina lake bado halijafahamika hadi alipotoa taarifa hiyo, lakini alisema anaendelea kupata matibabu.
Alisema taarifa za awali za kutokea kwa tukio hilo ni haraka ya wachimbaji hao kuingia mgodini kabla kupita muda wa saa 48 baada ya upigaji na ulipuaji wa baruti kufanyika mgodini.
Alisema kwa mujibu wa sheria na kanuni za madini zilizowekwa, wachimbaji wakipiga baruti katika miamba husubiri kwa muda wa saa 48, ili hewa nzito iweze kusambaa na hapo ndipo wanaruhusiwa ndani ya mgodi kuangalia madini.
“Sasa wachimbaji hao akiwamo marehemu na aliye mahututi hawakuwa na subira, waliamua kuingia mgodini kabla ya muda na kujikuta wakikutwa na mauti na mwingine kunusurika baada ya kukuta hali mbaya ya hewa,” alisema.
Aliwataka wachimbaji wote katika migodi kuheshimu taratibu zilizowekwa, ili kuepuka maafa na akawataka kuacha tamaa.
Social Plugin