Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe amesema licha ya madiwani wa chama hicho kujiuzulu kutokana na sababu mbalimbali, bado chama hicho kikuu cha upinzani nchini kina mtaji wa madiwani 1,132.
Kujivua uanachama kwa aliyekuwa diwani wa Chadema kata ya Nsalanga mjini Mbeya, mchungaji David Ngogo kumefikisha idadi ya madiwani 52 wa Chadema waliojiuzulu kutokana na sababu mbalimbali.
Ngogo alitangaza kujivua uanahama juzi na kubainisha kuwa amechukua uamuzi huo baada ya kutofautiana na viongozi wa Chadema kuhusu suala la maendeleo, ikiwa ni pamoja na uamuzi wake wa kumuomba Naibu Spika, Dk Tulia Ackson kusaidia maendeleo katika sekta ya elimu kwenye kata yake.
Idadi kubwa ya madiwani wa Chadema wamehamia CCM na wengi wao kupitishwa na chama hicho tawala kuwania tena nafasi hiyo jambo ambalo Mbowe ameeleza kuwa linaliingiza Taifa katika matumizi ya fedha yasiyo na msingi kwa chaguzi za marudio.
Mbowe alisema pamoja na hayo, Chadema bado ina mtaji wa madiwani wengi huku mkurugenzi wa itifaki, mawasiliano na mambo ya nje wa chama hicho, John Mrema akisema katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, Chadema kilipata madiwani 1,184 na sasa wamebaki 1,133 baada ya 51 kujiuzulu kwa kuhamia CCM na wengine kufariki dunia. Takwimu hizo zimefikia 1,132 baada ya Ngogo kujiuzulu juzi.
Diwani wa 51 kujiuzulu alikuwa Solomon Mmari (Nasai) takribani siku nne zilizopita.
Katika maelezo yake, Mbowe alisema hata kama wangeondoka madiwani watano, bado chama hicho na Watanzania wangeathirika na kusisitiza kuwa lazima wananchi wajiulize madiwani wanaojiuzulu wanafanya hivyo kwa staili ipi.
Miongoni mwa madiwani waliojiuzulu Chadema na kujiunga CCM, wamepitishwa kuwania tena udiwani katika uchaguzi wa ubunge na udiwani katika kata 77 unaofanyika Agosti 12 katika halmashauri 43 nchini.
Katika kata 23 ambazo awali zilikuwa zikishikiliwa na Chadema kabla ya madiwani wake kujiuzulu na kujiunga na CCM na kuteuliwa tena kuwania nafasi zao, wagombea wa Chadema wamekumbana na vizingiti ikiwa ni pamoja na kuwekewa mapingamizi.
Mbowe akizungumzia hilo alisema katika sehemu nyingi walizosimamisha wagombea wamekuwa wakienguliwa kwa sababu mbalimbali ikiwamo kutojua kusoma na kuandika na kukosea kujaza fomu.
Uchaguzi huo umetawaliwa na vitimbi ikiwamo baadhi ya wagombea kutoweka na kuzima simu; muhuri wa chama kufichwa na baadaye mhusika kujivua uanachama. Vingine ni mgombea kutuhumiwa kwa mauaji, mwingine kupewa mtihani wa kuandika neno “zinjanthropus.
Akizungumzia marudio ya chaguzi na kuenguliwa kwa madiwani hao kutokana na kukosa sifa, Mbowe alisema wanaoathirika si Chadema wala vyama vya upinzani pekee, bali Taifa kwa ujumla kwa kuwa wananchi wanakosa fursa ya kuchagua viongozi wanaowataka.
“Msiangalie Chadema peke yake kuwa itaathirika, bali Taifa pia litaathirika na hatua hii. Hizi fedha zinazotumika katika uchaguzi huu zingeenda kutumika katika miradi ya maendeleo kwa masilahi ya Watanzania,” alisema.
“Lakini fedha hizi zinatumika katika uchaguzi ambao wagombea ni walewale waliojuzulu chama kimoja na kuhamia kingine kwa sababu ambazo hazina kichwa wala miguu. Eti unamuunga mtu mkono kweli?” alisema mbunge huyo wa Hai.
Alidai kwamba sasa hivi kwenye chaguzi za marudio wagombea wa upinzani wanapigwa, wanatoweka, wananyang’anywa fomu mambo ambayo alisema hayajazoeleka na kwamba zamani walikuwa wakilalamikia wizi wa kura.
Mbowe alisema mambo hayo yana athari kwa Taifa na wananchi wenye mapenzi mema wanaopenda mabadiliko.
“Hili jambo linakandamiza demokrasia iliyopo. Pia tunaona nguvu kubwa inayotumika katika kuhakikisha ushindi unapatikana kwa CCM jambo ambalo linafanya demokrasia kudidimia.”
Siku nne zilizopita katibu wa itikadi, uenezi na mawasiliano kwa umma wa ACT-Wazalendo, Ado Shaibu alieleza kusikitishwa kwake na vitendo vya rafu na hujuma zinazoendelea katika mchakato wa uchaguzi huo mdogo wa marudio dhidi ya wagombea wa upinzani ambao wamekuwa wakitekwa na kutishiwa maisha.
Na Bakari Kiango, Mwananchi