Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan amesema Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Tunduma mkoani Songwe linastahili kuvunjwa kutokana na kutofanya vikao vyake kwa muda wa miezi tisa kinyume na tataribu na kanuni zake.
Alisema hayo jana katika mkutano wa hadhara uliofanyika viwanja vya Shule ya Msingi Mwaka mjini Tunduma wilayani Momba mkoani Songwe kuwa mgogoro uliojitokeza hadi baraza kutofanyika kwa muda mrefu unatokana na ukiukwaji wa kanuni na sheria uliofanywa na baraza hilo.
Alisema kwa mujibu wa sheria iwapo baraza la madiwani lisipokutana katika kipindi cha miezi mitatu linastahili kuvunjwa na kwamba atawasiliana na Waziri wa Tamisemi, Seleman Jafo ili kuona nini cha kufanya.
Makamu wa Rais alitumia nafasi hiyo kusisitiza umuhimu wa kufuata sheria na kuachana na matumizi mabaya ya madaraka kwa kuingiza maslahi binafsi.
Kuhusu wafanyabiashara waliohamia Zambia, alisema hakuna nchi yoyote ambayo haikusanyi kodi na kwa kuwa wao wameonyesha kukaidi sheria na hawataki kulipa kodi wabaki huko huko (Zambia) ambako kodi hazikusanywi.
"Tangu nimeingia mji wa Tunduma nimeona biashara nyingi sana na hivyo kuondoka kwa hao wametoa fursa nzuri kuwapisha wengine wenye uzalendo wa kulipa kodi ambazo ndiyo fedha zinazowaletea maendeleo" Alisema Samia
Kauli hiyo ilikuja baada ya Mbunge wa Tunduma (Chadema), Frank Mwakajoka kudai halmashauri hiyo hakuna demokrasia kufuatia baraza la madiwani kuzuiwa kufanya vikao kwa miezi tisa kutokana na kutoelewana kwa Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Ally Mwafongo na Mkuu wa Wilaya ya Momba, Jumaa Irando.
Alisema mgogoro ulianza baada Mwafongo kutangaza kuondoa ushirikiano na Irando kwa madai ya mkuu huyo wa wilaya alikuwa anaingilia mipango ya halmashauri, lakini baadae naye Irando akatumia mamlaka yake kuzuia madiwani hao kutofanya vikao vyote vya baraza hilo.
Pia aliwaagiza watumishi wote kuanzia maofisa watendaji wa mitaa, kata na halamshauri kutopokea maelezo au maagizo yoyote kutoka kwa madiwani hao.
Mwakajoka aliongeza kutokana na mahusiano mabaya baina ya Serikali ya wilaya na halmashauri na wafanyabiashara kudaiwa kodi kwa vitisho wafanyabiashara zaidi ya 2,000 wamehamia nchi jirani ya Zambia.
Kwa upande wake Mkuu wa mkoa Songwe, Chiku Galawa alisema mkoa umejipanga kuhudumia wananchi ambao wako tayari kushirikiana na Serikali kwa kulipa kodi ambayo ndiyo inayotumika kuwaletea maendeleo na kuwa walioondoka wasirudi na ikiwezekana eneo hilo litawekewa uzio ili wasirudi tena.
Social Plugin