MAKAMU WA RAIS AWAONYA WANAOKUFURU UUMBAJI WA MUNGU

Na Daniel Mwambene, Afisa Habari Ileje
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Mungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan amewaonya Watanzania kutokufuru uumbaji wa Mwenyezi Mungu kwa kuharibu mazingira ili kuendelea kulinda ikolojia.


Akizungumza na wananchi wa wilaya ya Ileje mkoani Songwe katika kijiji cha Sange mara baada ya kuzindua shamba la miti la Iyondo-Mswima katika eneo la Katengele Mhe. Suluhu alisema kuwa kuharibu mazingira ni kumkufuru Mungu.


“Kuharibu alichokileta Mungu kiwafae wanadamu huku mkiwa mnaenda misikitini na makanisani ni kumkufuru yeye”alisema kiongozi huyo. 


Alisikitishwa na shughuli za binadamu katika baadhi ya maeneo aliyoyapitia ndani ya wilaya ya Ileje ambako kilimo kinaendeshwa kando ya mito bila kujali sheria zinazolinda mito.


Mhe.Suluhu alisema kuwa iwapo sheria hizo hazitazingatiwa iko hatari ya milima mingi kubaki vipara kwani kinachofanyika si ukataji miti kwa malengo ya kutunza akiba bali ni unyoaji wa miti. 


Aliongeza kuwa kamwe kilimo kisiwe kisingizio cha kuharibu mazingira kwakuwa uharibifu wa mtu mmoja huleta madhara kwa wengi.


Awali kabla ya mkutano huo,Makamu wa Rais alizindua shamba la miti ambalo linaongeza idadi ya mashamba ya serikali huku likitarajiwa kutumia mamilioni ya pesa ambayo matokeo yake yataongeza ukubwa wa jina la Ileje kitaifa na kimataifa.


Akitoa taarifa Mkuu wa Wilaya ya Ileje Ndugu Joseph Mkude alisema kuwa wananchi wake ambao kwa asili ni wachapa kazi wamekuwa wakiitikia maagizo ya serikali vizuri ingawa wameonekana kufanya vibaya kwa kujiingiza katika imani za waganga wa jadi wajulikanao kama rambaramba. 


Viongozi wengine wa wilaya hiyo wakiwemo machifu,wachungaji na vyama vya siasa ngazi ya mkoa wa Songwe waliiomba serikali kuendelea kutatua kero ya miundo mbinu ya barabra ili kuwaongezea kasi ya maendeleo wananchi ambao kwa sasa wanashuhudia ujenzi wa barabara ya Mpemba-Momba hadi Isongole-Ileje kwa kiwango cha lami.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post