Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Freeman Mbowe akiweka jiwe la msingi kwenye jengo la ofisi ya Chama hicho Wilayani Tarime wakati wa uzinduzi wa kampeni za uchaguzi mdogo wa udiwani kata ya Turwa unaofanyika leo Julai 29, 2018. Picha na Waitara Meng'anyi - Mwananchi
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe ameagiza uongozi wa chama hicho kila wilaya kujenga ofisi ifikapo mwaka 2020 na kuondokana na kupanga.
Mbowe amesema hayo leo Jumapili Julai 29, 2018 wakati akiweka jiwe la msingi katika jengo la ofisi ya Chadema wilayani Tarime mkoani Mara.
Mwenyekiti huyo baada ya kukagua jengo la ofisi hiyo lenye vyumba vitatu, amesema mpango wa ujenzi wake ulicheleweshwa na huu haukuwa muda wake lakini akawapongeza viongozi walioona njozi ya kuanzisha ujenzi huo ambao uko hatua ya renta.
"Mimi naanza na Sh2 milioni kila mbunge mkoani Mara achangie milioni moja," amesema Mbowe.
Wabunge na wenyeviti wa halmashauri wamefikisha Sh10 milioni.
"Shughuli hii itasimamiwa na katibu wa chama mkoa, Chacha Heche ambaye ndiye mratibu wa mambo yote ya chama mkoa," amesema.
Awali, mwenyekiti wa Chadema wilaya ya Tarime, Lucas Ngoto akitoa taarifa fupi kuhusu upatikanaji na ujenzi wa jengo hilo la ofisi amesema: "Tulinunua uwanja huu mwaka 2012 kwa Sh6 milioni, lakini likiwa na mgogoro ambao uliisha baadaye.
“Mwaka huu mwezi wa pili tulianza ujenzi na kufikia hapa baada ya kukosa fedha ndani ya chama na fedha nyingine kutolewa na mbunge (wa Tarime Mjini), Esther Matiko, ili kukamilisha ujenzi huu tunahitaji Sh7 milioni, " amesema Ngoto.
Na Waitara Meng'anyi, Mwananchi
Social Plugin