Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MBOWE : WANAOFIKA BEI KWA AHADI YA FEDHA AU VYEO WAONDOKE MAPEMA CHADEMA



Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe amewataka viongozi, wanachama, wafuasi na wapenzi wa chama hicho kutotishika na wimbi la viongozi na wanachama wanaohamia vyama vingine akisema linakipa chama hicho fursa ya kujiimarisha.


“Wale wanaokimbilia vyama vingine wanakiimarisha zaidi chama chetu kwa sababu kinatupa fursa ya kubaki na viongozi na wanachama wenye uchungu na nia ya dhati ya kukijenga chama chao,” alisema Mbowe


Akihutubia mkutano wa kampeni kumnadi mgombea udiwani katika uchaguzi mdogo kata ya Turwa wilayani Tarime jana Julai 29, 2018 Mbowe alisema Chadema iko imara kulinganisha na wakati mwingine kutokana na kubakiwa na watu wenye nia ya dhati ya kukipigania.


“Wanaofika bei kwa ahadi ya fedha au vyeo waondoke mapema na ninawahakikishia Chadema itaendelea kuwa taasisi imara zaidi kuliko ilivyo sasa,” alisema Mbowe


Bila kutaja majina, kiongozi huyo alisema chama hicho kimewahi kuondokewa na viongozi wa ngazi za juu kiasi cha wengi kudhani kingeyumba lakini ikawa kinyume chake kwa kuimarika na kupata wabunge, madiwani na wachama wengi zaidi.


Viongozi wa kitaifa waliowahi kujiondoa Chadema ni aliyekuwa Katibu Mkuu, Dk Wilbrod Slaa na Makamu Mwenyekiti na Katibu Mkuu wa zamani Dk Amani Walid-Kaborou.

Kuhusu mgombea kata ya Turwa, Mbowe aliwaomba wapiga kura wa kata hiyo kutumia haki yao kikatiba kumchagua mgombea wa Chadema ili akaungane na madiwani wa chama hicho kuiongoza Halmashauri ya Wilaya ya Tarime inayopaa kimaendeleo tangu chama hicho kishike ushukani kulinganisha na ilipoongozwa na CCM.


"Shahada yako ndiyo ushindi wako, itumie kuleta mabadiliko kimaendeleo Tarime. Msiogope vitisho vya viongozi wa Serikali na vyombo vya dola na ninajua watu wa Tarime siyo waoga na hawarudi nyuma katika kile wanachokiamini,” amesema


Ili kuimarisha chama, Mbowe alitumia mkutano huo kuwaagiza viongozi wa Chadema kote nchini kuhakikisha wanahamasisha wanachama kujitolea kujenga ofisi za wilaya katika maeneo yao kukiwezesha chama hicho kuondokana na adha ya kupanga.


“Nimeweka jiwe la msingi la ofisi ya Chadema wilaya ya Tarime inayojengwa kwa nguvu na michango ya viongozi na wanachama; moyo huu uenee kote ili chama kiwe na ofisi zake za kudumu,”


Mbowe alichangia Sh2 milioni mbili kuunga mkono juhudi hizo na kuwaagiza wabunge wote na wenyeviti wa halmashauri zinazoongozwa na Chadema mkoa wa Mara kila mmoja kuchangia milioni moja.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com