MBUNGE STEPHEN NGONYANI 'MAJI MAREFU' AZIKWA TANGA

Spika wa Bunge Mheshimiwa Job Ndugai akiweka udongo katika mwili wa aliyekuwa Mbunge wa Korogwe Vijijini Marehemu Stephen Hillary Ngonyani katika mazishi yaliyofanyika leo kijijini kwake Kwamndolwa Wilayani Korogwe Jijini Tanga.
Spika wa Bunge Mheshimiwa Job Ndugai akizungumza wakati wa wa mazishi ya aliyekuwa Mbunge wa Korogwe Vijijini Marehemu Stephen Hillary Ngonyani yaliyofanyika leo nyumbani kwake Korogwe Jijini Tanga. kulia ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Ajira, kazi, Vijana na Wenye Ulemavu, Mhe. Jenista Mhagama na Kushoto ni Mufti Mkuu wa Tanzania, Sheikh Abubakari Zuberi
Mawaziri, Manaibu Waziri, Waheshimiwa Wabunge na Viongozi mbalimbali wa Kitaifa wakiwa katika mazishi ya aliyekuwa Mbunge wa Korogwe Vijijini Marehemu Stephen Hillary Ngonyani yaliyofanyika leo kijijini kwake Kwamndolwa Wilayani Korogwe Jijini Tanga.

Korogwe. Vilio, simanzi vimetawala leo Alhamisi Julai 5, 2018 katika mazishi ya aliyekuwa mbunge wa Korogwe Vijijini (CCM), Steven Ngonyani maarufu Profesa Majimarefu.


Wananchi waliozungumza na MCL Digital wamesema wamepoteza mtu muhimu kwa kuwa alikuwa anajua shida zao na amewasaidia katika masuala mbalimbali, ikiwa ni pamoja na maeneo yao kupata maji ya uhakika pamoja na barabara zinazopitika muda wote.


“Alikuwa akitujali wananchi wake. Alikuwa tofauti na wengine waliomtangulia. Alihakikisha vijana hawasumbuliwi kabisa katika biashara zao, hasa wanaoendesha bodaboda na bajaji,” amesema Ayubu Richard, mkazi wa Korogwe ambaye pia ni dereva bodaboda.


Mariam Salimu mkazi wa kijiji cha Kwamndolwa alikozikwa Majimarefu leo jioni, amesema katika kijiji hicho kulikuwa na shida ya maji lakini kupitia mbunge huyo sasa maji yanapatikana, “hata barabara ipo na inapitika.”


Msemaji wa familia ya marehemu, Hilary Ngonyani amesema familia ilikuwa ikimtegemea kwa kiasi kikubwa.


“Kama tungetakiwa kuchanga fedha ili ndugu yetu asifariki dunia tusingesita kufanya hivyo. Ila ukweli unabaki palepale kuwa jambo hilo haliwezekani kwa kuwa kila mmoja atafariki,” amesema.


Viongozi mbalimbali wameshiriki ibada ya mazishi ya mbunge huyo akiwemo Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Jenista Mhagama.

Habari imeandikwa na Rajabu Athumani, Mwananchi

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post