Mfanyabiashara wa madini ya dhahabu, Maliatabu Fugugu (50), mkazi wa Nyakato jijini Mwanza, anadaiwa kujiua kwa kujipiga risasi katika nyumba ya kulala wageni na mwili kukutwa ukiwa umeshikilia bastola.
Akithibitisha jana kwa njia ya simu, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita Mponjoli Lotosn, alisema tukio hilo limetokea Julai 20.
Akizungumzia mazingira ya tukio hilo, Kamanda Mpojoli alisema marehemu alikuwa mfanyabiashara wa madini ya dhahabu na kuwa chanzo cha kujiua bado hakijafahamika na kwamba uchunguzi bado unaendelea.
Kamanda Mpojoli alifafanua kuwa Maliatabu ambaye anamiliki miradi ya kuchakata na kuchenjua dhahabu katika machimbo ya Makaurugusi wilayani Chato mkoani Geita na Buhemba mkoani Mara, awali alikuwa mkazi wa Kijiji cha Lwamgasa kabla ya kuhamia Nyakato jijini Mwanza.
Inadaiwa Julai 19, alifika katika nyumba ya kulala wageni ya Flamingo iliyopo katika Kijiji cha Buselesele, wilayani Chato na kulipia chumba, lakini asubuhi wahudumu walikuta mlango umeegeshwa huku akiwa amekaa kwenye kiti
na walipomchunguza walibaini ameshafariki huku akitokwa damu na mkono wake wa kulia ukiwa umeshika bastola.
Alisema uchunguzi wa awali umebaini kuwa marehemu alijipiga risasi kifuani na kutokea upande wa kushoto karibu na sikio na katika bastola hiyo yenye uwezo wa kubeba risasi 10, kulikuwa na risasi tisa kwenye magazini, ikiwa
ni kiashiria risasi moja ilitumika.
Mwili wa marehemu umehifadhiwa katika Hospitali ya Wilaya ya Chato kwa hatua zaidi.
Kamanda aliiomba jamii kutafuta ufumbuzi wa matatizo kwa kushirikisha watu wa karibu au viongozi wa dini na wanandugu badala ya kuchukua maamuzi ya kujiua.
Matukio ya watu kujiua kwa kujipiga risasi yamekuwa yakijitokeza mara kwa mara katika sehemu mbalimbali nchini.
Hivi karibuni askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU), mkoani Tabora, alijipiga risasi akiwa katika sehemu yake ya kazi na kukatiza uhai.
Hata hivyo, chanzo cha kujiua askari huyo hakikufahamika mara moja na Jeshi la Polisi lilidai kuendelea na uchunguzi.
Katika tukio lingine lililotokea mkoani Mara, askari mwingine alijiua pia kwa kujipiga risasi kwa kile kilichoelezwa kuwa ni wivu wa kimapenzi.
Kufuatia vifo hivyo, Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP) Simon Sirro, ambaye alikuwa katika ziara ya kikazi mkoani Mara, aliomba viongozi wa dini kuingilia kati kwa kufanya ‘doria ya kiroho’ ili vifo vya aina hiyo visiendelee kutokea.
Social Plugin