Daniel
Homa (Chadema) aliyeteuliwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kugombea
udiwani kata ya Hayderer wilayani Mbulu mkoani Manyara amejitoa rasmi.
Kufuatia uamuzi huo, mgombea wa CCM, Justin Masuja amepita bila kupingwa.
Kujitoa
kwa Homa kumethibitishwa leo Julai 19, 2018 na msimamizi wa uchaguzi
jimbo la Mbulu Vijijini, Hudson Kamoga na kubainisha kuwa amepokea barua
ya kujitoa kwa mgombea huyo.
“Kwa
mamlaka niliyopewa kama msimamizi wa uchaguzi wa eneo hili, namtangaza
rasmi mgombea udiwani kwa tiketi ya CCM, Justin Masuja kuwa diwani
mteule anayesubiri kuapishwa baada ya kupita bila kupingwa," amesema
Kamoga.
Amesema
kwenye kata ya Tumati bado wanasubiri taarifa ya Tume ya Taifa ya
Uchaguzi (NEC) baada ya mgombea udiwani wa Chadema, Zacharia Nihhi
kuwekewa pingamizi na mgombea wa CCM.
"Mgombea
wa CCM, Paulo Axweso aliweka pingamizi kwa mgombea huyo wa Chadema
hivyo tunasubiria majibu kama ataruhusiwa au ataondolewa," amesema.
Akizungumzia kujitoa kwake, Homa amesema amechukua uamuzi huo kwa maendeleo ya Hayderer.
Amebainisha
kuwa hajashawishiwa na mtu yoyote kuachia nafasi hiyo, ameamua
kumuachia mgombea wa CCM ambaye awali alikuwa diwani wa kata hiyo kwa
tiketi ya Chadema.