Chama cha Wananchi (CUF) kimesema mwenyekiti wa kamati ya uongozi ya chama hicho, Julius Mtatiro amekamatwa na Polisi kutokana na ujumbe alioutuma katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa facebook unaodaiwa kumkejeli Rais John Magufuli.
Naibu Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na Mahusiano ya Umma wa chama hicho, Mbarala Maharagande katika taarifa yake kwa vyombo vya habari amesema Mtatiro amekamatwa jana Julai 5, 2018 na hadi sasa anashikiliwa na polisi.
Amesema mwenyekiti huyo katika ukurasa wake wa mtandao wa facebook ameandika, ‘rais kitu gani bwana’.
“Juzi Mtatiro alipokea simu ya wito wa kuhitajika kituo kikuu cha polisi Dar es Salaam. Jana alikuwa amealikwa kama mmoja wa wageni wawezeshaji wa mjadala na taasisi ya Twaweza katika kongamano la kujadili maoni ya wananchi kuhusu kushiriki maandamano na siasa,” amesema Maharagande.
“Ilipofika saa tatu asubuhi akiwa anaelekea huko alipigiwa simu kujulishwa afike kituoni hapo saa nne asubuhi. Niliambatana naye mpaka kituoni hapo na tulipokelewa na ZCO na kujulishwa kuwa anahitajika achukuliwe maelezo yake kuhusu ujumbe alioutuma katika mtandao huo.”
Amesema, “Tukakabidhiwa maofisa wa polisi wa kufanya kazi hiyo. Wakati wa kuanza kuchukuliwa maelezo yake alielezwa kuwa anatuhumiwa kwa kutuma ujumbe wa kejeli na kashfa dhidi ya Rais Magufuli kupitia mtandao wa kijamii.”
Amebainisha kuwa mwenyekiti huyu wa CUF upande unaomuunga mkono Katibu Mkuu wa chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad, alichukuliwa maelezo hadi saa 10 jioni, baadaye kuelekea nyumbani kwake kwa upekuzi.
Amesema walirejea tena kituoni hapo saa 4 usiku na maofisa wa polisi walimueleza kuwa wataendelea kuwa naye mpaka leo asubuhi, “Walisema watatujulisha kama watampatia dhamana au vinginevyo.”
Amebainisha kuwa Mtatiro amewataka wanachama wa CUF kutokuwa na hofu juu yake, wajitokeze kwa wingi mahakamani.
Chanzo- Mwananchi